Trump kuondoa hadhi inayolindwa kwa muda kwa Wasomali huku kukiwa na madai ya ulaghai huko Minnesota

(CRI Online) Januari 14, 2026

Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amesema kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X jana Jumanne kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anaondoa hadhi inayolindwa kwa muda kwa wahamiaji wa Somalia huku kukiwa na madai ya ulaghai katika Jimbo la Minnesota.

Shirika la Huduma za Uraia na Uhamiaji la Marekani limethibitisha taarifa hiyo kwenye mtandao wa X, likisema kwamba "kwa muda inamaanisha kwa muda," na kuongeza kuwa "raia wa Somalia wenye hadhi hiyo inayolindwa kwa muda sasa wanatakiwa kuondoka Marekani ifikapo Machi 17, 2026."

Marekani hutoa hadhi inayolindwa kwa muda kwa wahamiaji kutoka nchi fulani ambazo zimeathiriwa na hali zisizo za usalama, kama vile mapigano ya silaha yanayoendelea na majanga ya asili. Watu hao wanaweza kukaa kihalali nchini Marekani na kuomba idhini ya kufanya kazi.

Awali Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani ilitangaza kuondoa hadhi hiyo inayolindwa kwa muda kwa raia kutoka Afghanistan, Cameroon, Venezuela, Haiti, Sudan Kusini, Myanmar, Ethiopia, Nicaragua, Nepal na Honduras, na wengi wanakabiliwa na kesi au changamoto za mahakamani.

Wizara ya Sheria ya Marekani imeshtaki washtakiwa 98 katika kesi zinazohusiana na ulaghai katika jimbo hilo la Minnesota, 85 kati yao wakiwa na asili ya Somalia, kulingana na waraka wa hivi karibuni wa uhalisia wa mambo kutoka Ikulu ya White House.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha