Wang Yi asema ni wakati mwafaka kwa China na AU kuimarisha hali ya kuaminiana ya kimkakati na ushirikiano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2026

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi katika mahojiano na vyombo vya habari vya China Jumatatu baada ya kumaliza ziara yake katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Ethiopia, Tanzania na Lesotho amesema kuwa ni wakati mwafaka kwa China na AU kuimarisha hali ya kuaminiana kimkakati na kuzidisha ushirikiano wa kimkakati.

Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema China na AU, mtawalia ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea na jumuiya ya kikanda yenye idadi kubwa zaidi ya nchi zinazoendelea, zinapaswa kushirikiana kukabiliana na changamoto za sasa, si tu kulinda haki na maslahi halali ya China na Afrika, bali pia kutoa mchango wao katika amani na maendeleo ya dunia.

Kwa kuwa mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za Afrika, Wang amesema Mwaka wa Mawasiliano ya Watu kwa Watu kati ya China na Afrika, unaoonyesha mafanikio ya ushirikiano kati ya China na Afrika, utaunganisha vijana, utamaduni, vyombo vya habari na sekta nyingine kupitia karibu shughuli 600 za mawasiliano, zinazohusisha nyanja mbalimbali za mawasiliano kati ya China na Afrika.

Wang amesema kwamba alifurahishwa kuona mafanikio mapya ya maendeleo barani Afrika wakati wa ziara yake hiyo, na kwamba soko kubwa la China litatoa fursa pana zaidi kwa maendeleo ya Afrika.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutilia maanani zaidi na kuongeza uwekezaji barani Afrika.

Wang amesema China inapenda kushirikiana na nchi za Afrika kujenga majukwaa ya ushirikiano yaliyorasmishwa na kuziunga mkono kuchunguza kwa bidii njia za maendeleo zinazokidhi mahitaji yao halisi, kunufaisha umma kwa ujumla na kutumia kikamilifu rasilimali walizonazo.

"Ni pale tu China na Afrika zitakapoungana mikono kuelekea maendeleo ya mambo ya kisasa ndipo dunia itaweza kufikia maendeleo ya mambo ya kisasa. Bila maendeleo ya mambo ya kisasa ya Afrika, hakutakuwa na maendeleo ya mambo ya kisasa ya dunia," Wang amesema, akiongeza kuwa tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kilele wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika mwezi Septemba mwaka 2024, pande zote mbili zimeshirikiana kusukuma mbele utekelezaji wa matokeo yake.

"Hadi sasa, zaidi ya asilimia 90 ya malengo yamefikiwa au yamepata maendeleo chanya," ameongeza.

Wang amesema kwamba wakati wa ziara yake hiyo, marafiki wa Afrika wote wamesisitiza tena dhamira yao ya kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja na kuunga mkono juhudi za China za kufikia muungano wa taifa.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha