Lugha Nyingine
Iran yasema iko tayari kwa vita lakini imefungua mlango wa mazungumzo kufuatia tishio la Trump

Watu wakishiriki kwenye maandamano mjini Tehran, Iran, Januari 12, 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema nchi yake iko tayari kupigana vita lakini bado inapenda kufungua mlango wa mazungumzo, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema Jeshi la Marekani linafikiria "machaguo makali sana" kuhusu Iran huku kukiwa na machafuko ya sasa.
Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Al Jazeera Jumatatu wiki hii, Araghchi amesema, "Kama Washington inataka kujaribu chaguo la kijeshi ambalo iliwahi kulijaribu hapo kabla, tuko tayari kwa hilo," akiongeza kuwa anatumai Marekani itachagua mazungumzo.
Ameongeza kuwa mawasiliano na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff "yameendelea kabla na baada ya maandamano na bado yanaendelea."
Mahojiano hayo na Araghchi yanafuatia tishio la Trump la kutumia "machaguo kadhaa makali sana," ikiwa ni pamoja na uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Iran, katika kukabiliana na "ukandamizaji" wa Iran dhidi ya waandamanaji. Trump aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumapili kwamba maofisa wa Iran walikuwa wamewasiliana na Marekani ili kupendekeza mazungumzo, akiongeza kwamba "mkutano ulikuwa ukiandaliwa."
Maandamano yamezuka katika miji mingi ya Iran tangu Desemba 28. Hapo awali maandamano hayo yalianzishwa na wafanyabiashara wa soko moja la Tehran ambao walipinga kushuka kwa thamani ya fedha za rial za nchi hiyo, na mfumuko wa bei unaoongezeka, kabla ya kuenea hadi miji mingine. Machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu wa vikosi vya usalama na vya raia.

Watu wakishiriki kwenye maandamano mjini Tehran, Iran, Januari 12, 2026. (Xinhua/Shadati)
Machafuko hayo yamechochea madai ya watawala wa Iran kwamba Marekani na Israeli zinaweza kuwa nyuma ya pazia.
Katika mahojiano yake hayo na Al Jazeera, Araghchi pia ameelezea sababu ya Iran kufunga mtandao wa intaneti kufuatia machafuko hayo.
"Tumerekodi sauti za watu wakitoa amri kutoka nje ya nchi kwa maajenti wa magaidi, wakiwaagiza wawafyatulie risasi polisi na kuwafyatulia risasi waandamanaji kama polisi hawakuwepo. Nia yao ilikuwa kueneza mauaji," Araghchi amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



