Lugha Nyingine
Sudan yavipata tena vitu vya kale 570 vilivyoporwa wakati wa mgogoro wa kivita unaoendelea
![]() |
| Picha iliyopigwa Januari 13, 2026, mjini Port Sudan, Sudan, ikionyesha vitu vya kale vya kitamaduni vilivyopatikana tena ambavyo viliporwa wakati wa mgogoro wa kivita unaoendelea. (Picha na Sumaia Abdul Nabi/Xinhua) |
KHARTOUM - Serikali ya Sudan jana Jumanne ilitangaza kwamba imevipata tena vitu vya kale vya kitamaduni 570 vilivyoporwa wakati wa mgogoro wa kivita unaoendelea nchini humo, hii ni hatua muhimu ya Sudan katika kulinda mali za urithi wa kiutamaduni na utambulisho wa historia.
Akizungumza kwenye hafla ya kurudishwa kwa hivyo vya kale iliyofanyika Port Sudan, Graham Abdel Qader, naibu katibu mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Upashanaji wa Habari na Utalii ya Sudan ambaye pia ni mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi wa Utamaduni na Vitu vya Kale ya Sudan, ameuelezea upatikanaji huo tena kuwa ni "mafanikio makubwa ya kitaifa."
Amesema vitu hivyo vinahusisha vipindi mbalimbali vya historia, kuanzia nyakati za kabla ya historia hadi zama za sasa. Ameeleza kuwa kupatikana tena kwa vitu hivyo ni sehemu ya juhudi pana za kulinda mali za urithi wa kiutamaduni na kuhifadhi mali za urithi wa kihistoria za nchi hiyo.
Amesema mapitio ya hivi karibuni ya mali za makumbusho yameonesha upotevu wa vitu katika majumba kadhaa ya makumbusho, ikiwa ni pamoja na Jumba la Makumbusho la Gezira, ambalo lilipoteza vitu 68 kati ya 408, na Jumba la Makumbusho la Ethnographic, ambalo liliripoti idadi sawa na hiyo ya vitu vilivyopotea kutoka kwenye mkusanyiko wa vitu 4,600. Amesema vitu karibu 200 vya kale pia vimebainika kupotea kutoka Jumba la Makumbusho la Nyumba ya Khalifa, huku baadhi ya vitu vikiendelea kuwa mikononi mwa raia.
Abdel Qader ameongeza kuwa Jumba la Makumbusho la Kitaifa katika Mji wa Khartoum lilikumbwa na uporaji mbaya ikiwa ni pamoja na ukumbi wake mkuu wa maonyesho na majengo salama ya kuhifadhia vitu, na kusababisha kupotea kwa vitu 4,000 vya kale.
Ahmed Junaid Sorosh-Wali, mwakilishi wa UNESCO nchini Sudan, amesema kupatikana tena huko kwa vitu hivyo ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kimataifa katika kulinda mali za urithi wa kiutamaduni wakati wa migogoro ya kivita.
Tangu Aprili 2025, Sudan imekuwa ikishirikiana na INTERPOL na UNESCO ili kutafuta na kurudisha vitu ambavyo serikali hiyo inasema vilisafirishwa kwa magendo kutoka nchini humo kupitia majimbo mawili jirani.
Sudan imekumbwa na mgogoro mbaya wa kivita tangu Aprili 15, 2023, wakati mapigano yalipoanza kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan na wanamgambo wa Vikosi vya Uungaji Mkono wa Haraka, na kusababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na mamilioni kukimbia makazi yao ndani ya nchi au kuvuka mipaka yake.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




