Uganda yazima intaneti kabla ya uchaguzi mkuu

(CRI Online) Januari 14, 2026

Kamisheni ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), ambayo ni shirika la kitaifa la kudhibiti huduma ya mawasiliano, imezima mtandao wa intaneti nchini humo kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika kesho Alhamisi, Januari 15.

Mkurugenzi Mtendaji wa UCC Nyombi Thembo amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala jana Jumanne kwamba hatua hiyo imefuatia mapendekezo ya Kamati ya Usalama ya Mashirika Mbalimbali ya nchi hiyo.

Tangazo la kamisheni hiyo lililotolewa mapema Jumatatu wiki hii limesema mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo ya Usalama yanaeleza uwezekano wa matumizi ya mitandao kuzua taharuki wakati wa zoezi hilo.

Tangazo hilo limesema, hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti usambazaji wa habari potofu, ulaghai wa kura vilevile kuzuia uchochezi ambao unaweza kuathiri mshikamano wa kitaifa.

Kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kumeanza kutekelezwa jana Jumanne.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha