Maporomoko ya udongo yasababisha vifo vya watu wasiopungua 13 DRC

(CRI Online) Januari 14, 2026

Vyombo vya habari vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimeripoti jana Jumanne kwamba maporomoko ya udongo yaliyotokea usiku wa manane kuamkia tarehe 13 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 13 na wengine takriban 40 hawajulikani walipo.

Habari hizo zimesema maporomoko hayo yaliyotokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia tarehe 13, yamefunika nyumba nyingi kwenye kijiji kimoja huko Walikale katika Jimbo la Kivu Kaskazini, na kusababisha hasara kubwa kwa mali na maisha ya watu.

Kwa mujibu wa habari hizo, wakazi wenyeji wameanza kazi ya uokoaji, ambapo miili 13 imepatikana kwenye vifusi, wakiwemo watoto wanne. Vimeripoti kwamba hadi sasa, kazi ya uokoaji bado inaendelea, huku idadi ya vifo na majeruhi ikiwa na uwezekano wa kuongezaka zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha