Nchi mbalimbali zawataka raia wao kuondoka nchini Iran huku Iran ikifunga anga yake

(CRI Online) Januari 15, 2026

Wizara za Mambo ya Nje za Hispania, Italia na Poland zimetoa taarifa kwa nyakati tofauti kwenye tovuti zao, zikiwataka raia wao walioko nchini Iran kwa sasa kuchukua hatua zote iwezekanavyo kuondoka nchini humo haraka zikirejelea hali mbaya ya usalama katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Aidha wizara hizo zimewasihi raia wake wasisafiri kwenda Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa siku ya pili mfululizo, imewataka raia wake kuondoka Iran mara moja na kuwashauri kusafiri kwa njia ya ardhi hadi nchi jirani za Iran, Uturuki au Armenia.

Nayo serikali ya Uingereza Jumatano ilitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa ushauri wa kusafiri nje ya nchi ikitangaza kwamba kutokana na hali ya usalama, wafanyakazi wa Uingereza katika ubalozi wake nchini Iran wamerudishwa nyumbani kwa muda. Ushauri huo umesema ubalozi unaendelea kufanya kazi kutokea nje ya Iran.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Iran imetangaza kufunga anga yake kwa ndege zinazoingia au kutoka nchini humo isipokuwa zile zilizopewa idhini hapo awali.

Katika taarifa yake hiyo iliyotolewa jana Jumatano jioni, Iran imesema kwamba marufuku hiyo itaendelea kutumika kwa saa zaidi ya mbili hadi saa 10 alfajiri kwa saa za Tehran (0030 GMT), lakini inaweza kuongezwa muda wake.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha