Lugha Nyingine
Uzalishaji na Mauzo ya Magari ya China yafikia Viwango Vipya vya Juu Mwaka 2025

(Picha/VCG)
BEIJING - Takwimu zilizotolewa jumatano na Jumuiya ya Wazalishaji Magari ya China (CAAM) zinaonyesha kuwa, uzalishaji na mauzo ya magari ya China zimezidi magari milioni 34 mwaka jana, na kuweka rekodi mpya ya juu, zikitoa fursa mpya za ushirikiano na kusaidia kujenga mfumo wa kimataifa wa kunufaishana katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa CAAM, jumla ya uzalishaji magari ilifikia magari milioni 34.531 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.4 ikilinganishwa na mwaka 2024. Wakati huohuo mauzo ya magari yaliongezeka kwa asilimia 9.4 na kufikia magari milioni 34.4.
Jumuiya hiyo imeeleza kuwa, Uzalishaji na mauzo ya magari ya China zinaendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa miaka 17 mfululizo, na kwamba kwa miaka mitatu mfululizo uzalishaji na mauzo ya magari zimeendelea kuwa zaidi ya magari milioni 30 kwa mwaka.
CAAM imethibitisha kwamba magari yanayotumia nishati mpya (NEVs) yaliendelea kuharakisha kasi ya ukuaji, huku uzalishaji na mauzo zikifikia magari milioni 16.626 na milioni 16.49, mtawalia. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 29 na asilimia 28.2 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, na kuifanya China kuendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa miaka 11 mfululizo.
"Sekta ya magari ya China inaendelea kuonyesha uhimilivu na uhai mkubwa, huku viashiria vingi vikifikia viwango vipya vya juu, ikiashiria kukamilika kwa mafanikio kwa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025)," amesema Chen Shihua, naibu katibu mkuu wa CAAM.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mwaka jana China ilisafirisha nje magari milioni 7.098, ongezeko la asilimia 21.1 ikilinganishwa na mwaka 2024 .
Wataalam wamesema kuwa, takwimu hizo za mauzo ya nje ya China zinajumuisha mauzo ya nje kutoka kwa kampuni za ubia zinazofanya shughuli zao nchini China, hali ambayo inaonyesha kuwepo kwa mfumo wa kimataifa wa ushirikiano wa kunufaishana katika sekta hiyo.
Wataalam hao wamepinga madai ya kile kinachoitwa "uzalishaji wa kupita kiasi" katika sekta ya NEV, wakisema kwamba kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko, uwezo wa uzalishaji wa China haujazidi mahitaji, wala bado haujakidhi mahitaji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



