Lugha Nyingine
Raia 14 wauawa na wengine 14 kujeruhiwa katika shambulio linaloshukiwa kufanywa na kundi la wanaotaka kujitenga nchini Cameroon
Angalau raia 14, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa mapema jana Jumatano na wengine 14 kujeruhiwa wakati watu wanaoshukiwa ni wa kundi la wapiganaji wanaotaka kujitenga walipovamia jamii ya Mbororo katika Mkoa wa Kaskazini Magharibi wenye ghasia nchini Cameroon.
Akithibitisha tukio hilo, gavana wa eneo hilo, Adolphe Lele Lafrique, amesema shambulio hilo limetokea saa 11:30 alfajiri kwa saa za huko katika Kijiji cha Mbandfung cha tarafa ya Ndu kwenye eneo linalozungumza Kiingereza.
Naye meya wa Baraza la Ndu, Abdou Kanfon Borno amesema magaidi wanaotaka kujitenga walivamia kitongoji cha Gidado cha kijiji hicho, wakilenga jamii ya Mbororo inayoishi hapo.
Amefafanua kuwa hakukuwa na mapigano, kwani wanakijiji walikuwa bado wamelala na kwamba magaidi hao walimfyatulia risasi kila mtu, wakiwemo watoto na wanawake, ambapo mzee wa jamii hiyo anayeheshimika ameuawa.
Amesema, chanzo cha shambulio hilo bado hakijajulikana, na wapiganaji hao wanaotaka kujitenga bado hawajatoa taarifa yoyote.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



