Lugha Nyingine
Uchaguzi Mkuu wa Uganda waanza huku kukiwa na hali ya utulivu

Watu wakiwa wamepanga foleni kuchukua karatasi za kupigia kura kwenye kituo cha kupigia kura Wilaya ya Wakiso, Uganda, Januari 15, 2026. (Picha na Mary Kansiime/Xinhua)
KAMPALA - Uchaguzi Mkuu wa Uganda umeanza Alhamisi, huku wapiga kura zaidi ya milioni 21 wakipiga kura za kumchagua rais na wabunge chini ya ulinzi mkali. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, zoezi la kupiga kura lilipangwa kuanza saa 1 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki (04:00 GMT) na kufungwa saa 10 jioni.
Waganda zaidi ya milioni 21 wanatarajiwa kupiga kura ili kumchagua rais na wabunge 353 wanaochaguliwa moja kwa moja. Uchaguzi wa wabunge wanaowakilisha makundi yenye maslahi maalum, wakiwemo wazee, watu wenye ulemavu, wafanyakazi, na vijana, utafanyika baadaye.
Katika mji mkuu Kampala na sehemu nyingine za nchi hiyo, zoezi la kupiga kura lilicheleweshwa kutokana na hitilafu za mtandao zilizoathiri mashine za kuthibitisha wapiga kura kwa njia ya bayometria.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uganda, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda Simon Byabakama amesema maafisa wa uchaguzi wameelekezwa kutumia rejista za mikono kufuatia hitilafu hizo za kiufundi.
Wagombea wanane wanawania nafasi ya urais, akiwemo Rais aliye madarakani Yoweri Museveni, ambaye anagombea muhula wake wa saba wa miaka mitano.
"Ninawashukuru Waganda kwa kujitokeza na kupiga kura zao. Mashine za kuthibitisha wapiga kura zilikuwa na matatizo mwanzoni, lakini sasa zinafanya kazi vizuri," Museveni alisema muda mfupi baada ya kupiga kura katika wilaya yake ya nyumbani Kiruhura, magharibi mwa Uganda.
Mpinzani mkuu wa Museveni, nyota wa muziki wa pop aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi, alipiga kura yake huko Magere katika Wilaya ya Wakiso. Amewaambia waandishi wa habari kwamba licha ya kukamatwa kwa baadhi ya wafuasi wake, bado ana imani ya ushindi na aliwahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, mgombea urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali ili kushinda moja kwa moja. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa ndani ya saa 48 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa.
Waandishi wa habari wa Shirika la Habari la China, Xinhua walisema kuwa hali ya usalama jijini Kampala inaendelea kuwa kali lakini shwari, huku askari wenye silaha wakifanya doria kwa miguu na kwa kutumia vyombo vya usafiri.
Huku Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ikikosoa mchakato wa uchaguzi huo, ikitaja kukamatwa kwa wafuasi wa upinzani, serikali ya Uganda imekanusha madai hayo.

Robert Kyagulanyi, mgombea urais kutoka chama cha NUP (National Unity Platform), akipiga kura kwenye kituo cha kupigia kura katika Wilaya ya Wakiso, Uganda, Januari 15, 2026. (Picha na Mary Kansiime/Xinhua)

Mwanamke akipiga kura kwenye kituo cha kupigia kura jijini Kampala, Uganda, Januari 15, 2026 (Picha na Mary Kansiime/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



