WHO yaunga mkono juhudi za kukabiliana na kipindupindu za Malawi kwa kuipatia vifaa tiba vya dola milioni 182 za Marekani

(CRI Online) Januari 16, 2026

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeipatia Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Malawi vifaa tiba vyenye thamani ya dola milioni 182 za Marekani ili kusaidia nchi hiyo kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu unaoendelea na dharura za kiafya zinazohusiana na mafuriko ya hivi karibuni.

Kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana Alhamisi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe, Mwakilishi wa WHO nchini Malawi Neema Kimambo alisema uungaji mkono huo unalenga kuboresha vituo vya matibabu ya kipindupindu, maeneo ya kunywea maji, na vituo vya afya kwa watu walioathiriwa na mafuriko.

Amesema mchango huo unaendana na hatua zinazoendelea za serikali ya Malawi na kusaidia kushughulikia mahitaji ya dharura ya kiafya ya jamii zilizoathiriwa.

Naibu Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi Charles Chilambula ameipongeza WHO kwa uungaji mkono huo, pia kutoa wito kwa washirika wengine kuunga mkono mapambano dhidi ya kipindupindu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Chilambula, Malawi imerekodi wagonjwa 26 na kifo kimoja tangu Desemba 11, 2025.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha