Lugha Nyingine
Wakaazi wa Gaza wapokea "Bodi ya Amani" ya Trump kwa mashaka makubwa
GAZA - Wakaazi wa Ukanda wa Gaza wameeleza hali ya wasiwasi na mashaka makubwa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kuundwa kwa "Bodi ya Amani" ya kufanya uendeshaji wa Gaza, wakionya kwamba mpango huo unaweza kulazimisha kutekeleza usimamizi wa nje katika hali ambayo haijahakikisha ulinzi wa raia au usimamishaji mapigano wa kudumu.
Sameh Abu Marsa, mwenye umri wa miaka 40, ni mkaazi aliyekimbia makazi yake na kuishi kwenye kambi isiyo rasmi katika Jiji la Gaza, amesema tangazo hilo limezidisha hali yake ya wasiwasi.
"Niliposoma majina ya wajumbe wa Kamati ya Amani, nilihisi huu siyo mpango unaoyapa kipaumbele maslahi ya wakaazi wa Gaza," Abu Marsa amesema.
"Inaonekana zaidi kuwa ni aina mpya ya utoaji wa mamlaka ya kimataifa, ambao maamuzi yatatolewa nje na bila ushiriki kutoka kwa watu walio mashinani" ameongeza.
Amesema kuwepo kwa jina la mjumbe la Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair kunaleta wasiwasi zaidi kwa watu. "Usuli wa kisiasa wa Blair na ushiriki wake kwenye migogoro iliyopita vinaleta mashaka kwetu. Majina haya yanaonyesha biashara ya kisiasa badala ya amani ya kweli," ameongeza.
Huko Deir al-Balah katikati mwa Gaza, Hassan al-Hindi, mwenye umri wa miaka 50, baba wa watoto wanne ambaye nyumba yake imebomolewa katika mapigano ya hivi karibuni, amesema wakazi wa Gaza wameshuhudia mipango mingi ya kisiasa ikishindwa kuleta mabadiliko halisi.
"Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikia kuhusu mipango, mabaraza na mapendekezo, lakini hakuna chochote kilichobadilika kwenye ardhi hii ya Gaza isipokuwa uharibifu na hasara zaidi," amesema.
Ikulu ya White House Ijumaa ilitangaza wajumbe wa bodi hiyo, ikisema Rais Trump atakuwa ni mwenyekiti wake. Wajumbe wake ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, mjumbe maalum wa Trump Steve Witkoff, mkwe wake Jared Kushner, Blair na wengine.
Vuguvugu la Jihadi ya Kiislamu lilisema juzi Jumamosi kwamba linapinga "Bodi ya Amani," na linaona kuwa bodi hiyo inaendana na maslahi ya Israeli, na kutishia utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Israel pia imelalamika juu ya Washington kuunda chombo cha utendaji kusimamia utawala wa mpito wa Gaza bila uratibu kabla ya hapo.
Msemaji wa Hamas Hazem Qassem amesema "Bodi ya Amani," pamoja na kamati ya wataalam wa Palestina iliyotangazwa mapema wiki iliyopita mjini Cairo na nchi za Misri, Qatar, na Uturuki, zote hizo ni sehemu ya mpango wa Marekani wa kumaliza mgogoro.
Amesema mambo ya ndani ya Palestina lazima yabaki "mikononi mwa chombo kinachojitawala cha Palestina" na amesisitiza dhamira ya Hamas katika kuzuia kuibuka kwa mapigano mapya na kuhimiza kujenga upya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



