Huduma za Reli ya Zimbabwe-Msumbiji zasimamishwa kutokana na mafuriko

(CRI Online) Januari 29, 2026

Shirika la Reli la Zimbabwe (NRZ) limesema jana Jumatano kwamba limeifunga kwa muda njia ya reli ya Harare-Mutare baada ya treni moja kuacha njia katika Kijiji cha Odzi, Jimbo la Manicaland.

NRZ imesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii kuwa, kufungwa kwa njia hiyo, vilevile njia ya reli ya Chicualacuala-Maputo ambayo ilifungwa wiki mbili zilizopita, kunamaanisha kuwa kwa sasa hakuna usafiri wa treni kati ya Zimbabwe na Msumbiji.

Shirika hilo limesema kuwa, tukio hilo la treni kuacha njia yake limetokea baada ya sehemu ya reli hiyo kusombwa na mafuriko ya mvua kubwa iliyonyesha Jumapili iliyopita, ikiathiri mabehewa manne yaliyokuwa yamebeba ferrochrome kuelekea katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji.

NRZ imesema kufungwa kwa njia hizo mbili kutaathiri vibaya biashara kati ya nchi hizo mbili, vilevile usafiri wa kuelekea nchi jirani kama vile Botswana na Zambia.

Imeongeza kuwa kazi ya ukarabati itaanza baada ya kunyoosha na kuzipanga upya njia hizo za reli.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha