Lugha Nyingine
Hakuna mazungumzo chini ya shinikizo -- Iran yajibu juu ya tishio la Trump na vitendo vya kikosi cha majini cha Jeshi la Marekani Mashariki ya Kati

Picha hii iliyopigwa Januari 27, 2026 ikionyesha bango kubwa mjini Tehran, Iran. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Iran jana Jumatano ilikataa uwezekano wowote wa mazungumzo na Marekani ilimradi Washington inaendelea kutishia kuchukua hatua za kijeshi, na kabla ya hapo Rais wa Marekani Donald Trump aliongeza ukali wa maneno yake na kutangaza kupelekwa kwa vikosi vya kuongezwa vya majini vya Jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
"Hakutakuwa na mazungumzo katika hali yenye matishio," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi amesema, akinukuliwa na shirika la habari la IRNA linaloendeshwa na serikali ya Iran.
"Kufanya mambo ya kidiplomasia kwa kupitia shinikizo la kijeshi si jambo lenye ufanisi wala manufaa. Kama wanataka mazungumzo, lazima waache kutoa matishio, madai ya kupita kiasi, na masuala yasiyo na mantiki." amesema.
Katika maneno aliyoandika kwenye mtandao wa X, Araghchi ameongeza kuwa Iran inakaribisha makubaliano mapya kuhusu mpango wake wa nyuklia lakini itakabiliana vikali na operesheni yoyote ya kijeshi ya Marekani.
"Vikosi vyetu vya Jeshi jasiri vimejiandaa -- huku vidole vyao vikiwa kwenye kifyatulio," mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema.
Wakati huo huo, Trump ameihimiza Tehran kurudi kwenye mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia, akionya kwamba "kikosi kikubwa cha manowari" kinaelekea eneo hilo.
"Kikosi kikubwa cha manowari kinaelekea Iran," Trump ameandika kwenye jukwaa lake la mtandaoni la Truth Social, akiongeza kuwa kikosi hicho kitakuwa kikubwa zaidi kuliko kile kilichokuwa kimetumwa karibu na Venezuela na kitakuwa tayari kuchukua hatua katika wakati wa lazima.
"Natumaini Iran itakuja haraka mezani na kujadili makubaliano yaliyo ya haki na usawa –- kutotumia silaha za nyuklia," ameongeza.
"Muda unakaribia kukwisha." Trump ameonya kwamba kama hakutafikiwa kwa makubaliano, shambulio lolote la siku za baadaye la Marekani litakuwa "baya zaidi" kuliko vitendo vya kijeshi vilivyofanywa katika siku zilizopita.
Marekani tayari imetuma manowari ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln na manowari yanayobeba makombora ya kuongozwa katika eneo hilo. Kamandi ya Kati ya Marekani ilisema Jumatatu wiki hii kwamba kikosi cha manowari cha mashambulizi kinachoongozwa na manowari yenye uwezo wa kubeba ndege kimechukua nafasi katika maji ya Mashariki ya Kati, lakini hayakudokeza sehemu halisi kilipo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi (kulia) akihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Tehran, Iran, Januari 18, 2026. (Xinhua/Shadati)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



