Lugha Nyingine
Pengwini wa Afrika walio hatarini kutoweka watishiwa na homa ya ndege

Pengwini wa Afrika wakionekana ufukweni huko Simon, Cape Town, Afrika Kusini, Januari 24, 2026. (Xinhua/Deng Bingxue)
CAPE TOWN - Vyombo vya habari nchini Afrika Kusini vimeripoti kuwa mlipuko wa virusi vikali na hatari vinavyoeneza ugonjwa wa mafua miongoni mwa ndege wa porini (HPAI), ambao kwa kawaida huitwa ugonjwa wa mafua ya ndege, unatishia uhai wa ndege pengwini wa Afrika walio hatarini kutoweka ambao wanaishi kwenye pwani ya Afrika Kusini.
Mfuko wa Uhifadhi wa Ndege wa Pwani wa Afrika Kusini umesema pengwini 23 wa Afrika wamepimwa na kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo tangu Septemba 2025, huku pengwini angalau tisa wakithibitishwa kufariki miongoni mwa wale wanaoishi porini, habari zilizotolewa na vyombo vya habari zimesema Jumanne wiki hii.
"Kwa kundi la pengwini lililoko chini ya shinikizo kubwa, kupoteza hata wachache ni suala zito," mfuko huo ulisema kwenye shughuli ya kuadhimisha Siku ya Uhifadhi wa Pengwini iliyofanyika Januari 20.
"Mlipuko mkubwa ndani ya kundi hilo la kuzaliana utaleta athari kubwa sana kwa idadi ya pengwini wa Afrika inayopungua kwa kasi," SANCCOB ilisema.
SANCCOB imeuhimiza umma kutowagusa pengwini wagonjwa au waliokufa na kuripoti mara moja kwa mfuko huo au idara husika kuhusu hali waliyojionea juu ya pengwini.
Mwaka 2023, idadi ya pengwini wa Afrika (Spheniscus demersus) duniani kote ilipungua hadi kufikia chini ya jozi 10,000 za pengwini wa kuzaliana, na kusababisha Shirikisho la Uhifadhi wa Mazingira ya Asili la Kimataifa kuorodhesha spishi hizo kuwa "zilizo hatarini kutoweka" mwaka 2024.
SANCCOB ilisema mwezi Juni mwaka 2025 kwamba kwa hali ya hivi sasa, pengwini wa Afrika huenda wakatoweka porini ifikapo mwaka 2035.
Kwenye taarifa iliyotolewa Desemba 2025, mfuko huo ulisema pengwini zaidi ya 1,000 wa Afrika wamekufa kutokana na mafua hayo ya ndege tangu mwaka 2018.
Iliongeza kuwa kuanzia mwezi Julai 2025 zilikuwa na ripoti zilizosema kuwa pengwini 26 wa Afrika walikuwa wameshukiwa kuambukizwa HPAI, wakati huo ndipo mlipuko mpya wa ugonjwa huo mbaya ulipoanza kuathiri ndege wa baharini katika Jimbo la Western Cape la Afrika Kusini.

Pengwini wa Afrika wakionekana ufukweni huko Simon, Cape Town, Afrika Kusini, Januari 24, 2026. (Xinhua/Deng Bingxue)

Pengwini wa Afrika wakionekana ufukweni huko Simon, Cape Town, Afrika Kusini, Januari 24, 2026. (Xinhua/Deng Bingxue)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



