Lugha Nyingine
CRSG na Chuo cha Ufundi wa Reli cha Zhengzhou cha China wazindua akademia ya ufundi nchini Sierra Leone

Balozi wa China nchini Sierra Leone Zhao Yong (kushoto) na Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio wakihudhuria hafla ya uzinduzi wa akademia ya ufundi iliyojengwa kwa pamoja mjini Freetown, Sierra Leone, Januari 27, 2026. (CRSG/kupitia Xinhua)
FREETOWN – Kampuni ya kundi la saba la Shirika la Reli la China (CRSG), kwa ushirikiano na Chuo cha Ufundi wa Reli cha Zhengzhou cha China, zimezindua rasmi Akademia ya Ujuzi Bora Jumanne wiki hii katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown.
Mpango huo unalenga kuwapatia vijana wa Sierra Leone ujuzi muhimu wa ufundi, kuhimiza maendeleo ya vijana, na kuimarisha uhusiano kati ya China na Sierra Leone.
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa akademia hiyo, amesisitiza umuhimu wa mpango huo katika kuwezesha vijana, akiahidi uungaji mkono wa serikali na kuihimiza CRSG kupanua mchango wake, hasa kupitia kuanzisha vituo vya teknolojia vya China.
Balozi wa China nchini Sierra Leone Zhao Yong amewapongeza washirika hao kwa uzinduzi wa akademia hiyo alipohutubia hafla ya uzinduzi.
"Akademia ya Ujuzi Bora inabadili maono ya pamoja kuwa uhalisia," amesema, akifafanua kuwa mpango huo unaendana kwa karibu na ajenda ya serikali ya maendeleo ya vijana.
Zhao ameongeza kuwa mwaka 2026 unaadhimisha miaka 55 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Sierra Leone, pia ni Mwaka wa mawasiliano ya Watu kwa Watu kati ya China na Afrika. Amesema ubalozi wa China utaendelea kuunga mkono mawasiliano ya watu na ya kiutamaduni, vilevile ushirikiano wa kielimu kati ya nchi hizo mbili.
Samba Moriba, mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Freetown, amekaribisha mpango huo, akisema unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuendeleza mafunzo ya kiufundi na uwezo wa rasilimali watu.
"Mpango huu utahimiza mafunzo ya ujuzi miongoni mwa wanagenzi wetu na kutoa fursa za ujuzi, zitakazowawezesha kuchangia vyema kwa jamii," amesema.
Meneja Mkuu wa CRSG Du Xinguo amesema wanagenzi ambao watakamilisha mpango huo kwa mafanikio watapewa nafasi za kazi, zikiwawezesha kutumia ujuzi wao kazini.

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa akademia ya ufundi mjini Freetown, Sierra Leone, Januari 27, 2026. (CRSG/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



