Lugha Nyingine
China yatoa msaada wa sindano za insulini kwa wakimbizi wa Palestina nchini Jordan

Mkimbizi wa Palestina mwenye ugonjwa wa kisukari akitoa shukrani kwa msaada wa sindano za insulini uliotolewa na China kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Baqa'a nchini Jordan, Januari 28, 2026. (UNRWA/kupitia Xinhua)
AMMAN - China, kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Miradi kwa Wakimbizi wa Palestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), imetoa sindano za insulini kwa wakimbizi wa Palestina kwenye shughuli iliyofanyika Jumatano wiki hii katika Kambi ya Wakimbizi ya Baqa'a nchini Jordan.
Balozi wa China nchini Jordan Guo Wei amesema msaada huo unaonyesha uungaji mkono wa muda mrefu wa China kwa msaada wa ubinadamu kwa Wapalestina na uungaji mkono wake wa kila mara kwa UNRWA. Ameongeza kuwa China itaendelea kushirikiana na shirika hilo kupitia njia mbalimbali ili kuunga mkono kazi ya utoaji msaada wa ubinadamu ya Palestina.
Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Dunia na Ushirikiano wa Kusini na Kusini, utawanufaisha wakimbizi zaidi ya 43,000 wa Palestina katika sehemu mbalimbali za Kando za Magharibi za Mto Jordan, Gaza, Jordan, Lebanon, na Syria wanaohitaji matibabu ya insulini. Nchini Jordan pekee, sindano zaidi ya milioni 11 zitasambazwa, ambazo zitatosha kukidhi mahitaji ya wakimbizi wa eneo hilo wenye ugonjwa wa kisukari kwa mwaka angalau mmoja.
Raida Jawabreh, ambaye alikuja kuchukua sindano hizo, amesema kituo cha afya katika kambi hiyo hakikuwa na akiba kwa mwezi zaidi ya mmoja, hali ambayo ilimlazimu kununua sindano kutoka kwenye duka la dawa na kuzitumia kwa kurudiarudia ili kubana matumizi ya pesa. Amesema sasa anaweza kudongwa sindano ya insulini mara mbili kwa siku bila kutatizika.
Wakimbizi takribani 30,000 wa Palestina nchini Jordan wanaishi na ugonjwa wa kisukari, na takriban 14,000 wanahitaji sindano za insulini kila siku.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



