Lugha Nyingine
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aonya kwamba nguvu zinaibuka juu ya sheria duniani kote

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa mwanzo wa mwaka katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Januari 29, 2026. (Mark Garten/Picha za Umoja wa Mataifa/ kupitia Xinhua)
UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa nguvu zinaibuka juu ya sheria duniani kote, na kutoa wito wa kuharakishwa kwa mchakato wa dunia yenye ncha mbalimbali.
"Sheria ya nguvu inatawala juu ya nguvu ya sheria. Sheria ya kimataifa inakanyagwa. Ushirikiano unadorora. Na taasisi za pande nyingi zinashambuliwa katika pande nyingi," amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika mkutano na waandishi wa habari wa mwanzo wa mwaka uliofanyika jana Alhamisi.
"Tunaishi katika dunia ambayo vitendo - hasa vile vya ovyo - vinasababisha athari hatarishi. Athari hizo zinazidishwa na migawanyiko ya siasa za kijiografia na kukuzwa na janga la kutoadhibiwa." amesema Guterres.
"Wakati vitendo hatarishi havikutani na mwitikio unaostahili, mfumo huvurugika. Kutoadhibiwa ndiko kunakochochea migogoro ya leo -- kuongeza migogoro, kupanua hali ya kutokuaminiana, na kufungua milango kwa waharibifu wenye nguvu kuingia kutoka pande zote," amesema.
Guterres ametoa wito wa kufanyiwa mageuzi mfumo wa sasa ili kukabiliana na changamoto za kimataifa, hasa kupitia kuimarishwa kwa taasisi za mfumo wa pande nyingi.
"Ninapotazama wigo mzima wa changamoto za dunia, ukweli mmoja unaonekana wazi: mifumo yetu ya kushughulikia matatizo ya kimataifa inakabiliwa na wakati wa uamuzi. Mifumo hiyo imepitwa na wakati. Bado inaakisi miundo ya kiuchumi na nguvu ya miaka 80 iliyopita. Lakini dunia inasonga mbele," amesema.
"Hata hivyo miundo yetu, taasisi zetu, dhana zetu, na mitazamo yetu ya ushirikiano, bado imefungwa katika zama nyingine. Hili lazima libadilike," amesema.
Guterres amesema kwamba matatizo ya dunia hayatatatuliwa na nchi moja yenye nguvu kuamua kila kitu, wala nchi mbili zenye nguvu kuigawanya dunia katika nyanja hasimu za ushawishi.
Amesema Umoja wa Mataifa umeazimia kuchukua hatua zinazozalisha athari chanya na za kweli - athari za amani, haki, uwajibikaji, na maendeleo - katika nyakati hizi zenye misukosuko.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa mwanzo wa mwaka kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Januari 29, 2026. (Mark Garten/Picha za Umoja wa Mataifa/ kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



