Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum nchini Sudan wapokea ndege ya kwanza ya kibiashara katika karibu miaka 3

(CRI Online) Februari 02, 2026

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum Jumapili ulipokea ndege yake ya kwanza ya abiria ya kibiashara katika karibu miaka mitatu, ikiashiria hatua muhimu ya kuelekea kufungua tena uwanja huo na kurejesha usafiri wa kwenda mji mkuu wa Sudan baada ya kufungwa kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa shughuli za usalama wa anga katika uwanja huo wa ndege, Mohamed Jaafar Hassan, amesema ndege hiyo, inayoendeshwa na Shirika la Ndege la Sudan na kubeba abiria 160, iliwasili katika uwanja wa ndege huo ikitokea Port Sudan mashariki mwa Sudan.

Naye mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Viwanja vya Ndege vya Sudan, Bw. Al-Khatim Babiker Al-Tayeb, alisema katika taarifa kwamba uwanja wa ndege huo umeanza tena shughuli zake ukiwa na uwezo wa kutosha kwa kipindi hicho na unaweza kuhudumia hadi ndege nne kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa maandalizi ya kiufundi na kiusimamizi yanaendelea ili kuruhusu kurudi kwa safari za ndege za kikanda na kimataifa katika kipindi kijacho.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum uliharibiwa vibaya katika mzozo unaoendelea wa Sudan na ulikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza ya kushambuliwa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wakati mapigano yalipozuka mwaka 2023.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha