Kampuni za China zaingiza kasi katika mabadiliko ya kijani ya Afrika

(CRI Online) Februari 05, 2026

Nchi za Afrika zimetumia kikamilifu mitaji na utaalamu wa kiufundi kutoka kampuni za China ili kuhimiza matumizi ya nishati ya kijani, ikiwa ni pamoja na umeme unaotokana na nishati za jua, jotoardhi na upepo.

Hayo yamesemwa na watendaji waandamizi wa sekta ya nishati walipozungumza kwenye Mkutano wa Umeme Unaotokana na Nishati ya Jua wa Afrika “Intersolar Africa 2026”, ulioanza Jumanne wiki hii jijini Nairobi, Kenya.

Watendaji hao wamesifu jukumu ambalo kampuni za China zimebeba katika kusukuma mbele juhudi za kuondoa gesi ya kaboni kwenye sekta ya nishati ya Afrika.

“Kampuni za China zimekuwa zikichangia sana katika mabadiliko ya kijani kote barani Afrika. Ninaweza kusema zinakidhi matarajio yetu” amesema Cynthia Angweya-Muhati, kaimu afisa mtendaji mkuu wa Jumuiya ya Nishati Mbadala ya Kenya.

Amebainisha kuwa watengenezaji wa China wa suluhu za nishati ya jua wameanzisha minyororo imara ya usambazaji barani Afrika wakati huohuo wamefunza wasambazaji na wadau wengine katika mfumo wa ikolojia ya nishati ya kijani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Viwanda vya Kuzalisha Vifaa vya Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Jua ya Afrika Kusini, Rethabile Melamu, amesema ushirikiano na kampuni za China umehakikisha kwamba vipengele muhimu vya nishati ya jua, kama vile moduli, mifumo ya inverter, na miundo ya kupachika, vinapatikana katika soko la jumla.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha