Jopo la wawezeshaji wa Afrika lajadili mchakato wa amani wa mashariki mwa DRC

(CRI Online) Februari 05, 2026

Jopo la wawezeshaji la ngazi ya juu linaloongozwa na marais wa nchi za Afrika lilikutana Jumanne wiki hii mjini Kampala nchini Uganda, ili kusukuma mbele mchakato wa mazungumzo na amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkutano huo wa siku moja ulioongozwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ulikuwa na jukumu la kuunga mkono mazungumzo ya kikanda na kuimarisha miitikio ya pamoja katika kukabiliana na mgogoro huo wa mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Uganda jopo hilo limeshirikisha marais wastaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, wa Kenya Uhuru Kenyatta, wa Ethiopia Sahle-Work Zewde, wa Botswana Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi, na wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza.

Wakati akihutubia mkutano huo, Museveni alisema suluhu ya kudumu katika eneo la mashariki mwa DRC bado ni vigumu kupatikana. Naye Obasanjo amesisitiza haja ya kuwa na suluhu inayoendana na hali halisi ya Afrika, akibainisha kuwa mgogoro huo wa mashariki mwa DRC unahusiana na masuala mengi yanayohitaji kutatuliwa.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha