Xi asema yuko tayari kufanya kazi na Trump kuongoza meli kubwa ya uhusiano kati ya China na Marekani kusonga mbele kwa utulivu

(CRI Online) Februari 05, 2026

Rais wa China Xi Jinping amesema angependa kufanya kazi na Rais wa Marekani Donald Trump katika mwaka mpya ili kuongoza meli kubwa ya uhusiano kati ya China na Marekani kusonga mbele kwa utulivu kupita kwenye upepo na dhoruba, na kukamilisha mambo makubwa na mazuri zaidi.

Akizungumza jana Jumatano na Rais Trump kwa njia ya simu, Rais Xi amebainisha kuwa anaweka umuhimu mkubwa sana kwenye uhusiano kati ya China na Marekani, huku akisema kuwa mwaka uliopita, yeye na Trump walifurahia mawasiliano mazuri, na kufanya mkutano kwa mafanikio huko Busan, ambapo waliweka mwelekeo wa uhusiano kati ya China na Marekani.

Rais wa China amesema kuwa zote China na Marekani zina mambo muhimu katika ajenda zao mwaka huu, ambapo China itaanza Mpango wake wa 15 wa Miaka Mitano na kuandaa Mkutano wa Viongozi wa Kiuchumi wa APEC, na Marekani nayo itasherehekea maadhimisho ya miaka 250 tangu kupata uhuru wake pamoja na kuandaa Mkutano wa Viongozi wa G20.

Kwa upande wake, Trump amesema ana uhusiano mzuri na Xi na ana heshima kubwa kwake na kwamba chini ya uongozi wao, Marekani na China zinafanya vizuri katika nyanja kama vile uchumi na biashara.

Huku akibainisha kuwa anataka kuiona China ikifanikiwa, Trump amesema Marekani inapenda kufanya kazi na China na kupiga hatua zaidi katika uhusiano wa pande mbili.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha