Lugha Nyingine
Rais wa Rwanda Kagame atoa wito wa kuhimiza kuharakisha maendeleo na kufikia hali ya kujitegemea

Rais wa Rwanda Paul Kagame akizungumza kwenye mkutano wa 20 wa Baraza la Taifa la Mazungumzo, mjini Kigali, Rwanda, Februari 5, 2026. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)
KIGALI - Rais wa Rwanda Paul Kagame ametoa wito wa kufanya juhudi tena za kujitegemea na kuharakisha maendeleo ya nchi, wakati nchi hiyo ya Afrika ikianza mkutano wa 20 wa Baraza la Mazungumzo la Kitaifa.
Akifungua mazungumzo hayo mjini Kigali jana Alhamisi, Rais Kagame amesema Rwanda imepata maendeleo yanayoweza kupimika lakini lazima iharakishe kupiga hatua za kufikia malengo yake makubwa ya muda mrefu.
"Kwa nchi kama yetu, tukizingatia vyote changamoto tunazokabiliana nazo na fursa zilizopo kwetu, maendeleo yaliyopatikana bado hayajatosha. Lazima tupige hatua kubwa zaidi kuliko hapo kabla ili kupata maendeleo zaidi na kudumisha juhudi zetu na kujitahidi kupata maendeleo endelevu. " Rais Kagame amesema.
Rais huyo wa Rwanda ametoa wito wa kuwataka viongozi kwenye ngazi zote kuimarisha kazi za kubeba wajibu na kuwajibisha katika utoaji huduma za kiumma, akisisitiza kwamba uwajibikaji unapaswa kuimarishwa haraka katika serikali za mitaa na vitengo vyote vya kiserikali ili kuhakikisha utoaji huduma wenye ufanisi.
Amesisitiza kuwa, kujitegemea ni nguzo kuu ya mkakati wa maendeleo wa Rwanda, akihimiza raia kubeba wajibu wa pamoja kwa ajili ya mustakabali wa nchi, akisisitiza kwamba hadhi ya taifa na usawa kati ya nchi na nchi vinapaswa kuendelea kuwa kanuni ongozi.
Kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu wa Rwanda Justin Nsengiyumva alitoa ripoti juu ya hali ya utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa nchi hiyo wa kubadilisha muundo wa kazi husika.
Nsengiyumva amesema ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo uliendelea katika mwaka 2025, na wastani wa ongezeko ulifikia asilimia 8.7 katika robo tatu za kwanza.
Mazungumzo hayo, yanayojulikana nchini humo kwa jina la Umushyikirano, yamepangwa kuendelea hadi leo Ijumaa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali. Mazungumzo hayo yamewashirikisha wajumbe wa Baraza la Mawaziri na Bunge, wajumbe wa sekta binafsi, wanadiplomasia, viongozi wa serikali za mitaa, na Wanyarwanda kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya majadiliano kuhusu ajenda ya mabadiliko ya muundo, maendeleo ya uchumi, utawala wa nchi, na kushiriki kwa raia wa Rwanda.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akizungumza kwenye mkutano wa 20 wa Baraza la Mazungumzo la Kitaifa, mjini Kigali, Rwanda, Februari 5, 2026. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



