Lugha Nyingine
Shindano la Vipaji vya Muziki linaloungwa mkono na China laibua vipaji vya ubunifu wa vijana wa Kenya
NAIROBI - Fanuel Mulwa alikuwa mwenye furaha isiyo na kifani baada ya kuwashinda washindani kadhaa kwenye shindano la Imba kwa Afrika (Sing for Africa), kipindi cha vipaji vya muziki kinachoungwa mkono na China kilichozinduliwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya, mwezi Novemba 2025.
Msanii huyo alishindana katika kila sehemu ya shindano hilo, akivutia majaji kwa sauti yake laini, kujiamini, na uwezo wake wa kutawala jukwaa.
"Uzoefu ulikuwa mzuri, na wasanii walikuwa wenye ushindani mkubwa. Wakati wa mchujo, niliimba wimbo unaoitwa Kwaheri unaoeleza namna ya kusonga mbele na maisha mengine kutoka maisha ya awali ya kuvunjwa moyo," Mulwa aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kabla ya fainali, ambazo zilifanyika Februari 1.
"Kukutana na magwiji wa muziki wa Kenya wakati wa mchujo katika studio jijini Nairobi lilikuwa jambo la kutia moyo," amesema, akiongeza kuwa hali ya kutiwa moyo kutoka kwa majaji ilimsukuma kuboresha ufundi wake na kulenga ushindi katika shindano hilo lililovutia hadhira nchini Kenya na kwingineko.
Mulwa amesema uzoefu huo uliimarisha ujuzi wake wa kuandika nyimbo, na anapanga kutumia pesa za zawadi ya shilingi milioni moja za Kenya (dola za Marekani takribani 7,700) kuanzisha studio ili kukuza kizazi kijacho cha vipaji vya muziki nchini humo.
Shindano hilo la Imba kwa Afrika lililozinduliwa Novemba 12 na Chaneli ya Kimataifa ya Kituo cha Televisheni cha Hunan, China kwa ushirikiano na chombo cha habari cha Kenya, linalenga kukuza vipaji vya muziki vya vijana wakati huohuo likihimiza uhusiano wa kiutamaduni na urafiki kati ya China na Afrika.
Wasanii zaidi ya 500, akiwemo Mulwa, walihudhuria mchujo wa awali mwishoni mwa Novemba. Shindano hilo lilifanyika kwa sehemu tano, hadi kufikia fainali ya Februari 1.
Msanii huyo mahiri wa muziki aina ya neo-soul, Mulwa amesema shindano hilo pia limetoa jukwaa la kuimarisha mabadilishano ya kitamaduni kati ya China na Kenya ambayo yananufaisha wabunifu kutoka pande zote mbili.
Kutoka washindani karibu 500 katika mchujo wa awali, ni 21 pekee waliosonga mbele hadi raundi zilizofuata, huku watano hatimaye wakichaguliwa kwa fainali kuu. Kipindi hicho cha onyesho la vipaji na matukio yanayohusiana nacho pia ni sehemu ya shughuli muhimu zinazoadhimisha Mwaka wa 2026 wa Mawasiliano ya Kati ya Watu na Watu wa China na Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



