Lugha Nyingine
Afrika Kusini yapata dozi milioni 1 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na mdomo kwa mifugo
Mfanyakazi akionyesha chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na mdomo (FMD) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Februari 21, 2026. (GCIS/kupitia Xinhua)
JOHANNESBURG - Afrika Kusini imepokea dozi milioni moja za chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na mdomo kwa mifugo (FMD) zenye ufanisi mkubwa ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza milipuko ya mara kwa mara ya ugonjwa huo, Wizara ya Kilimo ya Afrika Kusini imesema.
Chanjo hizo, zilizonunuliwa kutoka kampuni ya dawa ya Argentina Biogenesis Bago, ni shehena ya kwanza kwa ajili ya utoaji chanjo wa kitaifa kwa awamu, huku dozi milioni tano zaidi zikitarajiwa kufika mwezi ujao wa Machi, wizara hiyo imeeleza.
Waziri wa Kilimo wa Afrika Kusini John Steenhuisen akifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari wakati akipokea rasmi shehena ya dozi za chanjo dhidi ya ugonjwa wa mguu na mdomo (FMD) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Februari 21, 2026. (GCIS/kupitia Xinhua)
"Kichupa hiki kidogo kitakuwa mwanzo wa sisi kuwezesha nyama nyekundu kuingia katika masoko kote duniani," Waziri wa Kilimo John Steenhuisen amesema wakati akipokea rasmi shehena ya dozi za chanjo hizo siku ya Jumamosi.
Amesema kuwa shughuli hiyo ya chanjo itaziwezesha mamlaka kuhama kutoka kukabiliana na mlipuko baada ya kuwa umetokea hadi usimamizi wa magonjwa kabla ya kutokea na ameeleza imani kwamba mpango huo wa chanjo utasaidia kudhibiti mlipuko wa sasa.
Afrika Kusini imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya mara kwa mara ya ugonjwa wa FMD katika miaka ya hivi karibuni, ikisababisha vizuizi vya kuuza nje na shinikizo kubwa kwa wafugaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Sera ya Chakula na Kilimo, kesi 24,400 za ugonjwa wa FMD katika mifugo ya nchi hiyo viliripotiwa katika mwaka 2025, ikizidi kwa kiasi kikubwa rekodi ya juu zaidi ya kesi 7,700 katika miaka 20 iliyopita zilizorekodiwa katika mwaka 2022. Milipuko hiyo imeathiri sana mauzo ya nje ya nyama ya ng'ombe ya nchi hiyo, ambayo yalifikia tani jumla ya 24,773 katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka 2025, ambayo ni kiwango cha chini kutoka tani 38,677 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.
Wafanyakazi wakisogeza chanjo dhidi ya ugonjwa wa mguu na mdomo (FMD) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Februari 21, 2026. (GCIS/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



