Lugha Nyingine
China yatathmini athari ya hukumu ya Mahakama Kuu ya Marekani kuhusu ushuru
BEIJING - Wizara ya Biashara ya China imesema Jumatatu kwamba imepata habari kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu ya Marekani juu ya ushuru wa serikali ya Marekani uliotozwa kwa kufuata Sheria ya Madaraka ya Kiuchumi Wakati wa Hali ya Dharura ya Kimataifa (IEEPA), na inafanya tathmini kwa pande zote juu ya maudhui husika na athari yake.
Mahakama Kuu ya Marekani ilitoa hukumu Ijumaa wiki iliyopita ikisema kwamba utozaji ushuru wa serikali ya Marekani kwa washirika wake wa biashara chini ya IEEPA ni kinyume cha sheria.
Wakati akijibu maswali ya vyombo vya habari, msemaji wa wizara hiyo amesema kwamba China siku zote inapinga aina zote za utozaji wa ushuru unaoongezwa wa upande mmoja, na kusisitiza kwamba hakuna washindi katika vita vya biashara na kujilinda kibiashara kutasababisha tu mwisho mbaya.
Msemaji huyo ameongeza kuwa, hatua hizo za upande mmoja wa Marekani, kama vile utozaji ushuru wa nyongeza na ushuru wa fentanyl, si kama tu zinakiuka sheria za uchumi na biashara za kimataifa lakini pia zinakwenda kinyume na sheria za ndani za Marekani, na hazilingani na maslahi ya upande wowote.
"China inaihimiza Marekani kufuta ushuru huo wa upande mmoja unaotozwa kwa washirika wa biashara," msemaji huyo amesema, akisisitiza kwamba China na Marekani zikifanya ushirikiano, zitanufaika pamoja; na China na Marekani zikifanya mapambano, zote zitapata hasara.
Msemaji huyo ameongeza kuwa China imeona kuwa upande wa Marekani unajiandaa kutumia hatua mbadala, kama vile uchunguzi wa biashara kwa kujaribu kudumisha ushuru huo uliotozwa kwa washirika wake wa biashara.
"China itafuatilia hili kwa karibu na kulinda maslahi yake kithabiti."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



