Safari za abiria za reli za China zafikia milioni 121 wakati wa likizo ya sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 25, 2026

BEIJING - Reli za China zimeshughulikia safari milioni 121 za abiria wakati wa likizo ya Mwaka Mpya wa Jadi iliyomalizika hivi punde, ikiwa na ongezeko la asilimia 11.5 ikilinganishwa na kipindi cha likizo hiyo hiyo ya mwaka jana, takwimu zilizotolewa jana Jumanne na Kundi la Kampuni la Shirika la Reli la China zinaonesha.

Takwimu hizo kutoka shirika hilo zinaonesha kuwa Jumatatu wiki hii, ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya likizo hiyo, reli za nchi hiyo zilishuhudia safari milioni 18.73 za abiria, na kuweka rekodi ya idadi ya juu kwa safari za abiria katika siku moja wakati wa sikukuu hiyo.

Shirika hilo limesema ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka, wastani wa treni 12,380 za abiria ziliendeshwa kwa siku, na treni 2,314 za abiria za kutoa huduma kwa muda ziliongezwa katika siku moja kwenye njia na sehemu zenye abiria wengi. Limesema, katika siku za kilele cha usafiri kabla na baada ya likizo hiyo, treni zaidi ya 1,000 za mwendo-kasi za kutoa huduma wakati wa usiku zilitoa huduma kila siku kwenye njia zenye wasafiri wengi.

Takwimu hizo zimebainisha kuwa, wakati wa likizo hiyo, mtandao wa reli wa China ulibeba tani milioni 85.38 za mizigo, huku wastani wa mizigo wa siku ukifikia mabehewa 157,000.

Sikukuu ya Spring, ambayo pia hujulikana kwa jina la Mwaka Mpya wa Jadi wa China, ilisherehekewa Februari 17 mwaka huu, na likizo rasmi ilidumu kwa siku tisa kuanzia Februari 15 hadi Februari 23. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha