Lugha Nyingine
MONUSCO yatuma ujumbe wa tathmini Uvira, DRC kufuatilia usimamishaji mapigano
KINSHASA, Feb. 24 — Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MONUSCO, jana Jumanne ulitangaza kupeleka ujumbe wa pamoja wa tathmini ya uchunguzi mjini Uvira, mji wa kimkakati mashariki mwa nchi hiyo, kuanzia Feb. 23 hadi 27, ili kujiandaa kwa ajili ya kuanzishwa kwa utaratibu wa pamoja wa kufuatilia usimamishaji mapigano.
Ukiwa umetumwa kama hatua muhimu ya mwanzo kwa upelekaji wowote wa siku za baadaye wa askari wa kulinda amani, ujumbe huo, ulioandaliwa kwa uratibu na Mkutano wa Kimataifa wa Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR), chombo cha kiserikali cha kikanda, unalenga kubaini iwapo mazingira ya kioperesheni yapo ili kuhakikisha mfumo wa ufuatiliaji ambao ni “wa kuaminika, salama na unaotekelezeka kioperesheni,” MONUSCO imesema katika taarifa.
Timu zilizowasili zinatarajiwa kutathmini hali ya ufikiaji wa maeneo, uhakikisho wa usalama, uwezo uliopo wa uchukuzi, pamoja na namna ya kushirikiana na wadau wenyeji mjini Uvira.
MONUSCO imesema ujumbe huo unafuatia mashauriano na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, ambaye pia ni mwenyekiti wa ICGLR, na ni sehemu ya mfumo wa usimamishaji mapigano uliotokana na makubaliano ya mfumokazi yaliyosainiwa na M23 mjini Doha, Qatar, Nov. 15, 2025.
Tangazo hilo la Umoja wa Mataifa linakuja huku kukiwa na mvutano unaongezeka katika eneo hilo la Uvira na nyanda za juu za Kivu Kusini ambako mapigano yanaendelea kati ya vikosi vya serikali na makundi washirika wake kwa upande mmoja na waasi wa M23 kwa upande mwingine, licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea.
Mapigano mapya yamekuwa yakiripotiwa tangu Jumatatu wiki hii katika maeneo ya migodini ya Rubaya, katika eneo la Masisi, Jimbo la Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, licha ya makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyopendekezwa na Angola ambayo yalipaswa kuanza kutekelezwa Feb. 18, mapigano makali yanayohusisha mashambulizi ya mizinga yalikuwa bado yanaendelea kuzunguka mji wa Rubaya asubuhi ya jana Jumanne.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



