Nchi za Afrika zatafuta kutumia kikamilifu soko la China la watalii wanaosafiri kwenda nje

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 26, 2026

Patricia de Lille (mbele, wa pili kushoto), Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini, akifanyiwa mahojiano mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Februari 24, 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Patricia de Lille (mbele, wa pili kushoto), Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini, akifanyiwa mahojiano mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Februari 24, 2026. (Xinhua/Chen Wei)

JOHANNESBURG - Wajumbe waliohudhuria mkutano wa Meetings Africa 2026, uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia Jumatatu hadi Jumatano, wametoa wito wa sera bora za visa, kuboresha miundombinu na masoko mahsusi ili kuvutia watalii wengi wa China barani humo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuzidisha mabadilishano ya kati ya watu na watu.

Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka nchi 21 za Afrika. Washiriki, wakiwemo maafisa wa utalii, wanadiplomasia na wadau wa sekta hiyo, wamesema kwamba China, moja ya vyanzo vikubwa zaidi vya watalii wanaosafiri kwenda nje duniani, inabaki kuwa soko muhimu la kimkakati kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa utalii wa bara hilo.

"Afrika Kusini imefanya majaribio ya mfumo wa Idhini ya Kusafiri ya Kielektroniki (ETA) kwa wasafiri wa China ili kurahisisha mchakato wa kutuma maombi," Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini Patricia de Lille ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, akiongeza kuwa mfumo huo ni "mwezeshaji mkubwa" katika kushughulikia vizuizi vya zamani vilivyosababisha muda mrefu wa kuandaa visa.

Akisema kuwa Afrika Kusini imepanga kuzindua kampeni nchini China ili kutangaza mfumo huo wa ETA huku ikishirikiana na mashirika ya ndege ili kuongeza safari za ndege, amesema kuwa kufuatia miaka miwili ya ushirikiano wa karibu na mamlaka za utalii za China, Afrika Kusini inalenga kuvutia "asilimia moja ya idadi ya watu wote wa China" kuwa watalii wa nchi hiyo.

Zaidi ya marekebisho ya sera, juhudi pia zinaendelea ili kuboresha huduma mahsusi. Amesema, serikali ya Afrika Kusini imeanzisha mafunzo maalum ya lugha ya Kichina kwa wataalamu wa utalii ili kuziba mapengo ya mawasiliano na kuboresha viwango vya huduma.

Kuzidisha ushirikiano kati ya Afrika na China katika miundombinu na biashara pia kunaingiza kasi mpya katika utalii.

Balozi Mkuu wa Zambia nchini Afrika Kusini Grace Mutembo amesema ushirikiano katika sekta za reli na uchukuzi umewezesha usafiri wa kibiashara na mapumziko.

Amebainisha kuwa Zambia imetangaza kikamilifu bidhaa zake za utalii katika maonyesho nchini China na kwamba miradi mikubwa ya miundombinu, ukiwemo wa kituo cha mikutano kilichojengwa na China, imeibuka kuwa alama mpya za kuvutia watalii wa kimataifa na kuunga mkono mawasiliano ya kitaalamu.

Kwa sasa, idadi inayozidi kuongezeka ya nchi za Afrika, yakiwemo maeneo maarufu ya utalii kama vile Mauritius, Shelisheli, Morocco, Tunisia, Madagascar na Misri, zimetoa ufikiaji wa bila visa au mfumo wa kupata visa wakati wa kuwasili kwa raia wa China.

Picha iliyopigwa Februari 24, 2026 ikionyesha hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Meetings Africa 2026 mjini Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)

Picha iliyopigwa Februari 24, 2026 ikionyesha hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Meetings Africa 2026 mjini Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha