Lugha Nyingine
Rwanda yapokea watafuta hifadhi 164 waliohamishwa kutoka Libya
Wizara ya Usimamizi wa Dharura ya Rwanda imesema nchi hiyo, kwa ushirikiano na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), imepokea watafuta hifadhi 164 waliohamishwa kutoka Libya siku ya Jumatano.
Takwimu za UNHCR zinaonyesha kuwa kundi hilo la hivi punde linafikisha jumla ya idadi ya watu 2,924, waliohamishiwa Rwanda tangu 2019 ambapo 2,585 tayari wamepewa makazi mapya katika nchi za tatu.
Wizara hiyo imesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa watafuta hifadhi hao wapya waliowasili ni pamoja na watu kutoka Eritrea, Sudan, Ethiopia, na Sudan Kusini, ambao wengi wao -- watu 143 -- wanatoka Sudan, ikifuatiwa na Eritrea yenye watu 19.
Imeongeza kuwa waliohamishwa watahifadhiwa kwa muda katika kituo cha mpito cha Gashora katika Wilaya ya Bugesera mashariki mwa Rwanda, ambapo watasubiri mchakato wa kuhamia nchi zingine.
Uhamisho huu ni kulingana na makubaliano ya maelewano yaliyosainiwa kati ya UNHCR na Umoja wa Afrika mwaka 2019, ambapo utaratibu huo wa kupitia Rwanda ulianzishwa ili kutoa ulinzi wa kuokoa maisha, msaada, na suluhu ya muda mrefu kwa wakimbizi waliokwama Libya kupitia uhamisho wa muda hadi Rwanda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



