Lugha Nyingine
Nchi za Ulaya zahimiza raia kuondoka Mashariki ya Kati kutokana na mvutano kati ya Marekani na Iran kuzidi kupamba moto

Picha hii iliyopigwa Februari 1, 2026 ikionyesha mandhari mjini Tehran, Iran. (Xinhua/Shadati)
BRUSSELS - Nchi zaidi za Ulaya zimehimiza raia wao kuondoka au kuepuka kusafiri kwenda Iran na maeneo mengine kadhaa ya Mashariki ya Kati kutokana na mvutano unaozidi kupamba moto kati ya Marekani na Iran.
Serikali ya Uingereza ilisema jana Ijumaa kuwa imewaondoa wafanyakazi wake kwa muda kutoka Iran, huku ubalozi wake ukiendelea kufanya kazi kutokea mbali, na imeshauri kutofanya safari za aina yoyote kwenda nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa pia imetoa ushauri wa usalama kwa raia wa Ufaransa dhidi ya kusafiri kwenda Israeli, Yerusalemu na Ukingo wa Magharibi, ikirejelea athari zinazowezekana za kikanda kutokana na hali inayoihusu Iran. Imeonya kuhusu uwezekano wa kufutwa au kucheleweshwa kwa safari za ndege na imehimiza raia katika maeneo yaliyoathiriwa kuendelea kuwa macho na kuepuka mikusanyiko.
Nchi nyingi za Ulaya zikiwemo Italia, Ujerumani, Poland, Finland, Sweden, Uholanzi, Serbia na zingine pia zimeonya raia wao dhidi ya kusafiri kwenda Iran na Israeli au kuhuisha ushauri wao wa kusafiri.

Vikosi vya majini vya Majeshi ya Israeli na Marekani vikishiriki kwenye mazoezi ya pamoja katika Bahari Nyekundu, Februari 1, 2026. (Vikosi vya Ulinzi vya Israeli/kupitia Xinhua)
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi imetoa ushauri wake wa kusafiri kwa maeneo ya mpaka kati ya Israeli na Gaza, Lebanon na Misri, ikirejelea kupamba moto huko kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.

Waandishi wa habari wakisubiri karibu na makazi ya balozi wa Oman mjini Geneva, Uswisi, Februari 26, 2026. (Xinhua/Lian Yi)
Manowari kubwa zaidi ya kubeba ndege za kivita ya Jeshi la Majini la Marekani, USS Gerald R. Ford, imewasili katika pwani ya Israeli siku ya Ijumaa, kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya raundi ya tatu yaliyokosa matokeo mazuri kati ya Washington na Tehran mjini Geneva, Uswisi.
Mvutano umekuwa ukipamba moto katika siku za hivi karibuni huku maafisa waandammizi wa Marekani wakionya mara kwa mara kuhusu uwezekano wa maingiliano ya kijeshi dhidi ya Iran.
Marekani imekusanya manowari mbili za kubeba ndege za kivita za mashambulizi, ndege zaidi ya 150 za kivita, zikiwemo ndege za kivita aina ya F-35, na imeimarisha kambi zake katika nchi za Jordan na Israel. Washington imeshawahamisha wafanyakazi wasio wa lazima kutoka ubalozi wake mjini Beirut.
Wakati huo huo, Iran imesema italipiza kisasi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo hilo iwapo itashambuliwa.

Picha hii iliyopigwa Februari 26, 2026 ikionyesha majengo ya makao makuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF) mjini Tel Aviv, Israeli. (Xinhua/Chen Junqing)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



