Magari ya pikapu yenye kutumia umeme yanayoungwa mkono na kampuni ya China yaingia barabarani Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 28, 2026

Picha iliyopigwa Februari 14, 2026 ikionyesha gari la pikapu la vyumba viwili vya kukaa abiria lenye kutumia umeme jijini Dar es Salaam, Tanzania. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Picha iliyopigwa Februari 14, 2026 ikionyesha gari la pikapu la vyumba viwili vya kukaa abiria lenye kutumia umeme jijini Dar es Salaam, Tanzania. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM – Mabadiliko ya Tanzania ya kuelekea usafiri wa kijani umepata msukumo mpya kutokana na kuwasili kwa magari ya kwanza ya pikapu (pickup trucks) yenye safu mbili za viti yanayotumia umeme nchini humo, ambayo yanawezeshwa na teknolojia na ushirikiano wa mnyororo wa usambazaji kutoka kampuni ya China.

Kampuni ya Magari ya Jenga Taifa Pamoja (JTP Auto), kampuni ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme ya Tanzania, imefanya kazi na kampuni ongozi ya kuunda vifaa asilia ya China (OEMs) kuanzisha magari yanayotumia umeme ya bei nafuu (EVs) yaliyoundwa kulingana na mazingira halisi ya Tanzania.

Amar Shangavi, mwanzilishi na afisa mtendaji mkuu wa JTP Auto, amesema kampuni hiyo ilichagua kwa makusudi kushirikiana na watengenezaji hao wa China kwa sababu ya uongozi wao duniani katika vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.

"China inaongoza katika teknolojia ya magari yanayotumia umeme. Kufanya kazi na OEMs huko kunaturuhusu kuunda magari kuendana na mazingira ya Tanzania wakati huohuo tukinufaika na utengenezaji mkubwa uliothibitishwa." Shangavi ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.

Ingawa mnyororo wa usambazaji umekita mizizi yake China, Shangavi amesema kwamba JTP Auto inamilikiwa na wanahisa wengi Watanzania na inalenga kujenga uwezo wa ndani. Kampuni hiyo inapanga kuanzisha shughuli za kuunganisha kikamilifu sehemu za magari yanayotumia umeme nchini Tanzania ndani ya miaka miwili, kwa ushirikiano na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam ili kutumia kikamilifu utaalamu wa uhandisi na kuharakisha uhamishaji wa teknolojia.

JTP Auto imeleta magari hayo ya pikapu yenye kutumia umeme kwani inalenga wateja wa kibiashara ambao wana uwezekano mkubwa wa kutumia teknolojia mpya kunapokuwa na faida dhahiri za kifedha.

Manufaa ya kuokoa gharama ni makubwa. Kwa mujibu wa data za kampuni hiyo, kuendesha gari linalotumia umeme nchini Tanzania ni nafuu kwa asilimia 86 kwa kila kilomita kuliko kuendesha gari linalotumia petroli.

Wakati gari la kawaida linaweza kusafiri kilomita takriban 10 hadi 15 kwa lita ya mafuta, gharama za umeme ni kama shilingi takriban 25 za Tanzania (dola takriban 0.01 za Marekani) kwa kila kilomita kwa gari linalotumia umeme, ikilinganishwa na shilingi takriban 200 kwa kila kilomita kwa petroli.

"Magari haya yameundwa kwa ajili ya mazingira halisi ya Tanzania, matumizi ya kibiashara, shughuli za kuyaendesha kwa makundi na uhakika wa kila siku, wakati huohuo yakileta uokoaji mkubwa wa gharama," Shangavi amesema.

Kampuni hiyo tayari imeshaweka vifaa vya kuchajia kwenye ofisi zake ili kuunga mkono kundi hilo jipya la magari yanayotumia umeme, ikitarajia matumizi mapana zaidi kadri miundombinu inavyozidi kupanuka.

Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, JTP Auto inapanga kupanua mtandao hadi kwenye shoroba muhimu za usafiri, zikiwemo za Chalinze, Bagamoyo, Tanga, Arusha, Dodoma na Iringa, kuwezesha usafiri wa nchi nzima wa magari yanayotumia umeme.

Serikali ya Tanzania imesema uungaji mkono kwa viwanda vya nchini humo na uwekezaji wa nishati safi. Magari ya EV yanaendana na vipaumbele vya kiuchumi vya nchi hiyo.

Jamaa akifanya jaribio la kuendesha gari la pikapu jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 14, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Jamaa akifanya jaribio la kuendesha gari la pikapu jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 14, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Jamaa akionyesha chaja ya gari la pikapu jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 14, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Jamaa akionyesha chaja ya gari la pikapu jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 14, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha