Lugha Nyingine
Idadi ya vifo yaongezeka hadi 148 katika shambulizi la Marekani na Israeli dhidi ya shule nchini Iran
TEHRAN - Idadi ya vifo kutokana na shambulizi la pamoja la Marekani na Israeli dhidi ya shule ya msingi ya wasichana katika jimbo la kusini mwa Iran la Hormozgan imeongezeka hadi kufikia 148, shirika la habari la Tasnim linalomilikiwa kwa sehemu na Serikali ya Iran, limeripoti jana Jumapili.
Shambulizi hilo pia limewaacha watu 95 wakiwa wamejeruhiwa, mwendesha mashtaka wa eneo hilo Ebrahim Taheri amenukuliwa akisema.
Amesema waathiriwa wengi wa shambulizi hilo la kikatili ni wanafunzi, huku walimu, wafanyakazi wa shule na wazazi wa wanafunzi pia wakiwa miongoni mwa waliouawa.
Juzi Jumamosi asubuhi, Israeli na Marekani zilianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine kadhaa ya Iran, ikiwemo Tabriz, Qom, Isfahan, Kermanshah, na Karaj. Iran ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na droni zilizolenga Israeli na kambi za Marekani katika nchi mbalimbali za eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Mashambulizi hayo dhidi ya Tehran yamemuua Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei, Katibu wa Baraza la Ulinzi la nchi hiyo Ali Shamkhani na Mohammad Pakpour, kamanda mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



