Wang Yi afanya mazungumzo na mwenzake wa Russia juu ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 02, 2026

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jana Jumapili alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Rssia Sergei Lavrov ambapo amesema kwamba chini ya msukumo wa China na Russia, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lilifanya kikao cha dharura juzi Jumamosi juu ya hali ya sasa nchini Iran.

"China bila kuyumbayumba imekuwa ikishikilia malengo na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kupinga matumizi ya nguvu katika uhusiano wa kimataifa," Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema.

Wang amesema haikubaliki kwa Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran wakati wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani, na ameongeza kuwa pia haikubaliki kwa nchi hizo kumuua waziwazi kiongozi wa taifa lenye mamlaka na kuchochea mabadiliko ya serikali.

Wang amesema kwamba vitendo hivyo vinakiuka sheria ya kimataifa na kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa.

Huku akibainisha kupamba moto huko kwa mgogoro kumeenea katika eneo zima la Ghuba ya Uajemi, Wang amesema kwamba hali hiyo katika Mashariki ya Kati inaweza kusukumwa kwenye shimo hatari, na China ina wasiwasi mkubwa kuhusu hilo.

Wang amesema kwamba msimamo wa China kuhusu hali hiyo nchini Iran ni kama ifuatavyo: Kwanza, kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi, pili, kurejea haraka kwenye mazungumzo na majadiliano, na tatu, upingaji wa pamoja wa hatua za upande mmoja.

Kwa upande wake, Lavrov amesema kwamba mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yameharibu sana utulivu katika Mashariki ya Kati.

Amesema Russia ina msimamo sawa na China na iko tayari kuimarisha uratibu na mawasiliano na upande wa China ili kutuma ishara dhahiri kupitia majukwaa kama vile Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, akitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita na kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha