Lugha Nyingine
Uchumi wa China wasonga mbele na kupiga hatua mpya yenye sifa bora zaidi katika mwaka 2025
BEIJING - Takwimu mpya zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) zinaonyesha kuwa uchumi wa China umeendelea kuwa imara licha ya changamoto na mazingira magumu mwaka jana, ikifikia ukuaji tulivu wa Pato la Taifa (GDP) wa asilimia 5 kutoka mwaka uliotangulia na kupiga hatua mpya yenye sifa bora zaidi katika sekta za kiuchumi na kijamii.
Hatua hiyo iliyopigwa imeimarisha zaidi jukumu la China la kuwa mchangiaji na mtulizaji muhimu wa uchumi duniani.
"Takwimu hizi mpya zilizotolewa zinaonyesha mafanikio makubwa katika maendeleo ya uchumi wa China mwaka uliopita," amesema Sheng Laiyun, naibu mkuu wa NBS, akibainisha kuwa takwimu hizo zinaonesha picha ya jumla ya uchumi wa China, wenye sifa ya ufanisi tulivu, mwendo mzuri na uhimilivu mkubwa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, jumla ya uchumi wa China iliendelea kupanda juu zaidi katika mwaka 2025, ikizidi yuan trilioni 140 (dola za Marekani takribani trilioni 20.22) kwa mara ya kwanza, na kufikia lengo la maendeleo kwa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025).
Takwimu hizo zinaonyesha kwamba katika mwaka wa 2025, Pato la Taifa kwa kila mtu la China lilifikia yuan 99,665, au dola 13,953 za Marekani kwa kiwango cha wastani wa ubadilishaji sarafu wa mwaka, na kuendelea kubaki juu ya dola 13,000 za Marekani kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, ikichochewa na uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia, tija ya kazi iliongezeka kwa asilimia 6.1 katika mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, asilimia 1.1 juu zaidi kuliko ukuaji wa Pato la Taifa.
"Kwa kuwa na ukuaji wa Pato la Taifa wa asilimia 5 na kuchangia asilimia takribani 30 ya upanuzi wa uchumi duniani, China inaendelea kuwa mchocheaji na mtulizaji mkuu wa uchumi duniani," Sheng amebainisha.
Amesema ikiwa ni soko la pili kwa ukubwa duniani la uagizaji bidhaa kutoka nje kwa miaka 17 mfululizo na kutoa uwekezaji endelevu wa kwenda nje, China imechangia gawio lake la maendeleo na dunia na kutimiza wajibu wake kwenye maendeleo duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



