Lugha Nyingine
Watu 6 wameuawa na kadhaa wakwama katika ajali ya kuporomoka kwa jengo jijini Johannesburg

Picha iliyopigwa Machi 2, 2026 ikionyesha jengo lililoporomoka jijini Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)
JOHANNESBURG – Watu wasiopungua sita wameuawa na wengine kadhaa bado wanakwama baada ya jengo kuporomoka jana Jumatatu kwenye mtaa wa kusini mwa Johannesburg, Afrika Kusini, mamlaka za Afrika Kusini zimesema.
Msemaji wa Idara ya Huduma za Dharura ya Johannesburg Xolile Khumalo amewaambia waandishi wa habari kwenye eneo la tukio kwamba watu wawili wamethibitishwa kukwama chini ya vifusi, huku wengine watatu wakiwa bado hawajulikani walipo. Amesema, mtu mmoja ameokolewa kwa mafanikio.
“Tukio limetokea katika Eneo Maalum la Kibiashara la Amethyst huko Ormonde, ambapo wafanyakazi 12 walikuwa kwenye ghorofa ya chini ya jengo la ghorofa mbili wakati sehemu ya jengo hilo ilipoporomoka,” amesema Khumalo.
Mamlaka zimeutaka umma kuepuka eneo hilo ili kuhakikisha shughuli za dharura zinaendelea kwa usalama.
Zimesema juhudi za utafutaji na uokoaji zinaongezeka. Waokoaji wamebainisha kuwa changamoto kuu inayozikabili timu hizo ni kutokuwa na utulivu wa jengo hilo, wakionya kwamba sehemu za jengo hilo "tayari zinaanguka."
Maafisa wamesema shughuli zitaendelea hadi watu wote wasiojulikana walipo watakapopatikana.
Sababu za kuporomoka kwa jengo hilo bado hazijajulikana katika hatua ya sasa, na uchunguzi unaendelea.

Watu wakifanya kazi kwenye eneo la jengo lililoporomoka jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Machi 2, 2026. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



