Lugha Nyingine
Japan yaweka makombora ya masafa marefu kwa mara ya kwanza bila ya kujali upingaji (4)
![]() |
| Wakazi wakiandamana kupinga hatua ya serikali ya Japan ya kuweka makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kujibu mashambulizi katika maeneo ya Kumamoto na Shizuoka, Tokyo, Japan, Machi 31, 2026. (Xinhua/Yue Chenxing) |
TOKYO - Wizara ya Ulinzi ya Japan imesema kwamba makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kujibu mashambulizi yamewekwa kwa mara ya kwanza kwenye vituo viwili vya Kikosi cha Kujilinda cha Ardhini (GSDF) nchini humo, hatua ambayo imesababisha upingaji kutoka watu wa nchini humo.
Shirika la Habari la Kyodo limeripoti kuwa uwekaji huo wa makombora kwenye Kambi ya Kengun katika Eneo la Kumamoto, kusini magharibi mwa Japan, na Kambi ya Fuji katika Eneo la Shizuoka, katikati mwa Japan, unaonesha mabadiliko makubwa yametokea katika sera ya kujihami kabisa ya nchi hiyo inayotekelezwa kwa muda mrefu kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ya kuacha vita.
Kambi ya Kengun imewekewa makombora ya aina ya 12 yaliyoboreshwa ambayo yanaweza kurushwa kutoka ardhini dhidi ya manowari baharini, na yanaweza kuruka kwa umbali wa kilomita takriban 1,000, yakivuka mipaka ya ardhi ya Japan na kuonekana dhahiri kuwa na uwezo wa kufanya mashambulizi.
Wakati huo huo, makombora ya kasi ya juu yamewekwa kwenye kitengo cha mafunzo kwenye Kambi ya Fuji. Makombora hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya ulinzi wa kisiwa, baada ya kurushwa, umbali wa kuruka kwake unaweza kufikia kilomita mia kadhaa, na wizara hiyo iko katika juhudi za kuuboresha hadi kufikia umbali wa kilomita takriban 2,000.
Shirika hilo la Habari la Kyodo limesema, Japan imekuwa na "uwezo wa kujibu mashambulizi dhidi ya kituo cha adui" kabla ya uharibifu halisi kutokea, kama ingechambua na kutambua kwamba shambulio liko karibu. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kwamba maamuzi yenye makosa yana hatari ya kukiuka sheria ya kimataifa na kuwa shambulio linaloanzishwa kwanza nayo.
Atsushi Koketsu, profesa wa heshima katika Chuo Kikuu cha Yamaguchi cha Japan, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba ingawa serikali inauelezea uwezo huo kuwa ni mbinu ya kutoa onyo na tishio kubwa, lakini "ni wazi unazidi wigo wa kujihami."
Siku ya Jumanne wiki hii, wakazi wenyeji wa Kumamoto walifanya maandamano karibu na Kambi hiyo ya Kengun, wakiwa na mabango yaliyoandikwa "Pinga uwekaji" na "Hatutaki makombora," Shirika la Habari la Kyodo liliripoti.
Waandamanaji hao wameeleza wasiwasi kwamba uwekaji huo wa makombora unaweza kulifanya eneo hilo kuwa shabaha la kijeshi la kulengwa , na wamekuwa wakitoa wito mara kwa mara kwa wizara ya ulinzi ya Japan kufanya mkutano wa hadhara wa kutoa maelezo yao kwa umma, lakini mkutano huo bado haujafanyika, ripoti hiyo ilisema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




