Lugha Nyingine
Wanaanga wa Artemis II waipita rekodi ya umbali uliofikiwa na Apollo 13 (3)
![]() |
| Picha iliyopigwa Aprili 6, 2026 ikionyesha Mwezi ukionekana kutoka kwenye chombo cha anga ya juu cha Orion. (NASA/kupitia Xinhua) |
LOS ANGELES – Wanaanga wa jukumu la Artemis II la kusafiri kwenye anga ya juu jana Jumatatu wamevunja rekodi ya umbali mrefu zaidi kutoka Duniani kuwahi kufikiwa na wanadamu, wakiipita hatua muhimu iliyofikiwa na jukumu la Apollo 13 mwezi Aprili 1970, kwa mujibu wa NASA.
NASA imesema, hatua hiyo muhimu imefikiwa majira ya saa 7:56 mchana kwa Saa za Mashariki (1756 GMT).
Wanaanga hao wanne ni kamanda wa NASA Reid Wiseman, rubani Victor Glover, mtaalamu wa jukumu la safari ya anga ya juu Christina Koch, na mtaalamu wa jukumu wa Shirika la Anga ya Juu la Canada (CSA) Jeremy Hansen. Jukumu la safari hiyo ya anga ya juu lilianzishwa kutoka Kituo cha Anga ya Juu cha NASA cha Kennedy katika jimbo la Florida nchini Marekani Aprili 1.
Wanaanga wa Apollo 13 waliweka rekodi ya awali ya kufika umbali wa maili 248,655 (kilomita karibu 400,171) Aprili 15, 1970, ambapo walichukua mwelekeo wa dharura wa kurudi duniani kihuria kuzunguka Mwezi baada ya mpasuko wa tanki la oksijeni kutatiza mpango wao wa kutua mwezini.
Wanaanga hao wa jukumu la Artemis II walikiita chombo chao cha anga ya juu cha aina ya Orion jina la “Integrity” (Uadilifu) kabla ya jukumu la safari yao hiyo. Wanaanga hao walisema jina hilo linaakisi maadili ya imani, heshima, udhati, na unyenyekevu ambayo wanayaona kuwa muhimu kwa uchunguzi wa anga ya juu ya kina. NASA imetumia jina hilo la Integrity kuwa ishara ya wito wa chombo hicho katika kipindi kizima cha jukumu la safari hiyo.
Wakati wa kupita mwezi, mwanaanga wa CSA Hansen aliwaarifu wasimamizi wa jukumu hilo kwamba wanaanga hao walikuwa wakipendekeza majina ya kreta mbili zisizo na majina kwenye Mwezi. Wanaanga hao wamependekeza kuipa jina la Integrity kreta ya kwanza ya mwezi ambalo ni jina la chombo chao cha anga ya juu.
Artemis II kinafuata mwelekeo wa kurudi duniani kihuria kama ule uliotumiwa na Apollo 13. Chombo hicho cha Integrity kinatarajiwa kufikia umbali wake wa kikomo cha juu wa maili 252,760 kutoka Duniani saa 1:07 jioni kwa Saa za Mashariki kabla ya kuanza kurudi.
Jukumu la safari hiyo halijumuishi kutua mwezini. Kutua kwenye maji kwa chombo hicho kurudi duniani kumepangwa kufanyika Aprili 10 katika Bahari ya Pasifiki karibu na San Diego, California.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




