Idadi ya wanunuzi wa kigeni yafikia rekodi mpya kwa kipindi cha kwanza cha Maonyesho ya Canton ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 20, 2026
Idadi ya wanunuzi wa kigeni yafikia rekodi mpya kwa kipindi cha kwanza cha Maonyesho ya Canton ya China
Mnunuzi akiangalia chombo kidogo cha matumizi ya nyumbani katika Maonyesho ya 139 ya Uagizaji na Uuzaji Bidhaa Nje ya China, Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, Aprili 19, 2026. (Xinhua/Lu Hanxin)

GUANGZHOU – Waandaaji wa maonesho hayo wamesema, Kipindi cha kwanza cha Maonyesho ya 139 ya Uagizaji na Uuzaji Bidhaa Nje ya China, ambayo pia yanajulikana kwa jina la Maonyesho ya Biashara ya Canton, kimefungwa rasmi jana Jumapili, ambapo idadi kubwa ya wanunuzi kutoka nchi mbalimbali duniani imeweka rekodi mpya.

Kituo hicho kimesema, hadi kufikia saa 11 jioni jana Jumapili, wanunuzi wapatao 167,000 kutoka nchi na maeneo 216 walikuwa wameshiriki kwenye maonyesho hayo nje ya mtandao, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.9 kuliko ile ya kipindi kama hicho cha maonyesho yaliyopita.

Kimesema kuwa, idadi hiyo ya wanunuzi, ambayo ni ya juu zaidi kuliko ile ya kipindi chochote cha kwanza cha maonyesho hayo yaliyopita, imeonesha uhimilivu na nguvu hai ya biashara ya nje ya China. Kipindi hicho cha kwanza cha maonyesho hayo chenye kaulimbiu ya "kusukuma mbele maendeleo ya utengenezaji bidhaa," kimeweka vibanda zaidi ya 25,000, na waonyeshaji bidhaa wamefikia zaidi ya 12,000.

Maonyesho hayo ya mwaka huu yanafanyika katika vipindi vitatu nje ya mtandaoni katika Mji wa Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, na yataendelea kufanyika hadi Mei 5. Kipindi cha pili, kilichopangwa kuanza Aprili 23 hadi 27, kitaweka mkazo wa kuonesha "maisha bora ya nyumbani," ikiwa ni pamoja na raslimali za ujenzi, samani, vyombo vya matumizi ya nyumbani, zawadi na mapambo.

Maonyesho hayo ya biashara ya Canton yaliyoanzishwa rasmi mwaka 1957, yanafanyika mara mbili kila mwaka katika Mji wa Guangzhou. Ni maonyesho yanayofanyika kwa muda mrefu zaidi kati ya shughuli za biashara ya kimataifa zinazofanyika nchini China, na zimekuwa zikisifiwa kuwa kipimo cha biashara ya nje ya China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha