Mabaki ya askari wahanga 12 wa China katika Vita vya Korea yarudishwa nyumbani kutoka Korea Kusini (7)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 23, 2026
Mabaki ya askari wahanga 12 wa China katika Vita vya Korea yarudishwa nyumbani kutoka Korea Kusini
Majeneza yenye mabaki ya askari wahanga wa Jeshi la Kujitolea la Watu wa China yanayosindikizwa na kikosi cha ulindaji yakikaribia kuwekwa kwenye gari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taoxian, Shenyang, Mkoa wa Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, Aprili 22, 2026. (Xinhua/Li Gang)

SHENYANG - Mabaki ya askari 12 wahanga wa Jeshi la Kujitolea la Watu wa China (CPV) waliopoteza maisha yao wakati wa Vita vya Kupinga Uchokozi wa Marekani na Kuisaidia Korea (1950-1953) yamerudishwa China kutoka Korea Kusini jana Jumatano.

Ndege kubwa ya usafirishaji ya Y-20B ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Ukombozi wa Umma la China iliyokuwa imebeba mabaki ya askari hao waliouawa na vitu vyao binafsi 146 ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taoxian huko Shenyang, mji mkuu wa Mkoa wa Liaoning wa kaskazini mashariki mwa China.

Baada ya kuingia anga ya China, ndege hiyo ya usafirishaji ya Y-20B ilisindikizwa na ndege nne za kivita za J-20. Baada ya kutua kwenye uwanja huo wa ndege, ilipewa saluti ya maji katika kutoa heshima kwa mashujaa hao waliofariki.

Kikosi cha ulindaji kilichobeba majeneza kilipotoka kwenye ndege hiyo, hafla ya kutoa rambirambi ilifanyika kwenye uwanja wa ndege, ambapo watu zaidi ya 1,800, wakiwemo wajumbe kutoka jeshini, maveterani wa vita, na jamaa za askari wahanga wa CPV wameshiriki kwenye hafla hiyo.

Majeneza hayo yalikuwa yamefunikwa kwa bendera ya taifa la China, na washiriki waliinamisha vichwa mara tatu kwa ukimya mbele ya mabaki ya wahanga hao. Mabaki hayo yatazikwa kwenye makaburi ya askari wahanga katika mji huo wa Shenyang leo Alhamisi.

Miaka zaidi ya 70 iliyopita, CPV ilivuka Mto Yalu na kushirikiana bega kwa bega na jeshi na raia wa Jamhuri ya Watu ya Kidemokrasia ya Korea (DPRK) kupigana vita dhidi ya jeshi la Korea Kusini na vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyokuwa vikiongozwa na Marekani. China ilituma wanajeshi milioni 2.9 wa CPV kuisaidia DPRK wakati wa vita hivyo, ambapo miongoni mwao zaidi ya 360,000 waliuawa au kujeruhiwa. Askari wengi wa CPV waliofariki walizikwa kwenye Rasi ya Korea.

Kutokana na makubaliano kati ya China na Korea Kusini yaliyosainiwa mwishoni mwa mwaka 2013, pande hizo mbili zinashauriana kila mwaka kuhusu makabidhiano ya mabaki ya askari hao wa China yaliyogundulika katika nchi ya Korea Kusini.

Tangu mwaka 2014, China na Korea Kusini zimekamilisha makabidhiano 13 mfululizo yaliyohusu mabaki ya askari wahanga 1,023 wa CPV.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha