Hifadhi ya Taifa ya Kruger ya Afrika Kusini yaadhimisha miaka 100

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 01, 2026
Hifadhi ya Taifa ya Kruger ya Afrika Kusini yaadhimisha miaka 100
Ndege cape glossy starling akionekana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Kruger katika Jimbo la Mpumalanga, Afrika Kusini, Mei 31, 2026. (Xinhua/Chen Wei)

SKUKUZA - Hifadhi ya Taifa ya Kruger ya Afrika Kusini Ijumaa jioni iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya sherehe ya kufikisha karne moja kwenye Kambi ya Mapumziko ya Skukuza chini ya kaulimbiu ya "Urithi Wetu, Mustakabali Wetu."

Shughuli hiyo iliwakutanisha maafisa wa serikali, wawakilishi wa jamii na wadau wa uhifadhi zaidi ya 100 ili kusherehekea urithi na mustakabali wa moja ya maeneo maarufu zaidi ya Afrika yanayolindwa.

Akihutubia kusanyiko hilo, Waziri wa Misitu, Uvuvi na Mazingira wa nchi hiyo Willie Aucamp amesema kwamba karne hiyo ya kwanza ya Kruger ilijengwa juu ya uhifadhi, utafiti wa kisayansi na utalii, huku karne yake ya pili pia itajumuisha sehemu ya nne - ushiriki wa jamii.

Pia ameelezea matumaini kwamba vizazi vijavyo vitaendelea kufurahia maajabu ya mazingira ya asili ya hifadhi hiyo, kuanzia kutazama tembo wakivuka Mto Sabie hadi kusikia simba wakinguruma msituni wakati wa usiku.

Kabla ya sherehe hiyo, Aucamp aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha juhudi za uhifadhi katika miaka ijayo.

Alisema Afrika Kusini inakaribisha uungaji mkono kutoka kwa washirika kote duniani, ikiwemo China, hasa katika maeneo kama vile uhifadhi wa wanyamapori na utafiti wa kiteknolojia.

Kruger iliyoanzishwa mwaka 1926 chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa za Afrika Kusini, ni hifadhi ya kwanza ya taifa ya nchi hiyo na moja ya maeneo makubwa zaidi ya Afrika yanayolindwa.

Ikichukua eneo lenye ukubwa wa hekta takriban milioni 2 katika majimbo ya Limpopo na Mpumalanga, ni nyumbani kwa spishi zaidi ya 300 za miti, na spishi zaidi ya 140 za mamalia na spishi 500 za ndege, zikiwemo za "Wanyama Wakubwa Watano" maarufu (Big Five), yaani simba, chui, tembo, faru na nyati.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha