Afrika CDC na WHO wazindua mpango wa kujiandaa na kukabiliana na Ebola kwa bara zima

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 08, 2026

Wafanyakazi wakiandaa milo kwa watu walio chini ya karantini, Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 4, 2026. (Xinhua)

Wafanyakazi wakiandaa milo kwa watu walio chini ya karantini, Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 4, 2026. (Xinhua)

ADDIS ABABA/GENEVA - Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wamezindua mpango wa kujiandaa na kukabiliana mlipuko wa Ebola kwa bara zima, wakilenga kuratibu juhudi za kudhibiti mlipuko huo.

Wakihutubia mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mtandaoni siku ya Ijumaa, wakuu wa Afrika CDC na WHO wamesema kwamba mpango huo mpya uliozinduliwa utatumika kama mfumokazi ulioratibiwa kuunga mkono nchi zinazoathiriwa, kuimarisha hali ya kujiandaa na kulinda usalama wa afya wa Afrika.

Mpango huo unalenga kukusanya dola milioni 518 za Marekani ili kuunga mkono nchi za Afrika kujiandaa, kwa ajili ya kubaini ugonjwa kwa haraka na kukabiliana na mlipuko huo kwa kipindi cha kati ya Juni na Novemba 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus akifanya ziara Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 31, 2026. (Xinhua)

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus akifanya ziara Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 31, 2026. (Xinhua)

Mkurugenzi Mkuu wa Afrika CDC Jean Kaseya amesema kwamba mpango huo wa pamoja "unalipa bara njia dhahiri ya kuchukua hatua kwa kasi na umoja ili kuokoa maisha, kuunga mkono nchi zilizoathiriwa, na kulinda jamii jirani."

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, kwa upande wake, amesisitiza hitaji la haraka la kuongeza ushirikiano kati ya nchi zinazoathiriwa na zilizo hatarini vilevile washirika wa bara hilo na wa kimataifa.

"Kudhibiti Ebola kunategemea dhamira ya kisiasa, ufadhili endelevu na imani na ushiriki wa jamii," Tedros amesema. "Mpango huu unaweka jamii katikati, kwa sababu bila ushiriki wao, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wanaoshukiwa kuambukizwa utakwama, huduma salama zitacheleweshwa, na maambukizi yataendelea."

Mpango huo wa miezi sita unawaleta pamoja serikali, washirika na jamii chini ya mbinu iliyounganishwa ya "Kukabiliana kwa Umoja" ili kuimarisha hatua za kukabiliana na mlipuko, ikiwemo uratibu wa dharura, ufuatiliaji wa ugonjwa, upimaji kwenye maabara, kuzuia na kudhibiti maambukizi, huduma ya kliniki, ushiriki wa jamii, utafiti, usambazaji wa vifaa na uungaji mkono kwa huduma muhimu za afya.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha