Kombe la Dunia lafunguliwa Mexico City huku mwenyeji Mexico na Korea Kusini ziking’ara katika mechi za Kundi A

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 12, 2026
Kombe la Dunia lafunguliwa Mexico City huku mwenyeji Mexico na Korea Kusini ziking’ara katika mechi za Kundi A
Wasanii wakitumbuiza kwenye sherehe ya ufunguzi wa Kombe la Dunia la FIFA 2026 katika Uwanja wa Mexico City, Mexico, Juni 11, 2026. (Xinhua/Li Muzi)

MEXICO CITY - Kombe la Dunia la FIFA 2026 limeanza rasmi usiku wa Alhamisi kuamkia leo Ijumaa kwa hafla ya ufunguzi katika Uwanja wa Azteca ambayo ilisherehekea utamaduni wa Mexico na kurejea kwa mashindano hayo katika uwanja huo wa kihistoria.

Katika mechi ya kwanza kabisa ya Kundi A ya mashindano hayo, mwenyeji Mexico ameanza kampeni yake ya kusaka ubingwa kwa kuibuka kidedea baada ya kuichapa Afrika Kusini kwa mabao 2-0 kwa magoli yaliyofungwa na Julián Quiñones katika dakika ya 9 tu ya mchezo na lile la Raúl Jiménez katika dakika ya 67.

Mechi ya pili ya kundi hilo imeshuhudia Korea Kusini ikiichakaza Jamhuri ya Czech 2-1. Katika mechi hiyo iliyokuwa yenye kasi muda wote huku milango ikiwa migumu kufunguka, hatimaye Czech ilifungua pazia la magoli kwa bao la kuongoza lililofungwa na Ladislav Krejčí katika dakika ya 59 ya mchezo. Hata hivyo dakika nane tu baadaye, Hwang In-beom aliisawazishia Korea goli hilo kabla ya Oh Hyeon-gyu kuihakikishia Korea goli la ushindi katika dakika ya 80.

Mashindano hayo yataendelea leo usiku tena, kwa saa za Afrika Mashariki kwa mwenyeji mwingine Canada kuchuana na Bosnia na Herzegovina huku mwenyeji mwingine wa tatu Marekani akimenyana na Paraguay.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha