Lugha Nyingine
Iran na Marekani zote zadai ushindi juu ya makubaliano ingawa kuna migongano ya kina kati yao

Picha hii iliyopigwa Juni 7, 2026 ikionyesha Mnara wa Amani ukiwa na jengo la Bunge la Marekani, the Capitol, mjini Washington, D.C., Marekani. (Xinhua/Li Rui)
TEHRAN/WASHINGTON - Marekani na Iran zote mbili zimedai ushindi baada ya kusaini makubaliano kwa njia ya kidijitali juzi Jumatatu yanayolenga kumaliza mgogoro ulioendelea kwa miezi mitatu, lakini kila upande kati ya pande zote mbili unaendelea kutoa maelezo yanayokinzana na maudhui ya makubaliano hayo ambayo bado hayajatangazwa hadharani.
Iran imeyaita makubaliano hayo ni ushindi wake dhidi ya Washington na Israeli.
"Adui aliyeshambulia kwa kutimiza kusudi lake ovu ameshindwa kufikia malengo yake yote, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata ushindi mkubwa katika vita," Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi alisema katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni ya serikali Jumatatu.
Rais wa Marekani Donald Trump amepongeza makubaliano hayo kwa kurejesha utulivu kwa masoko duniani.
"Nadhani mambo mengi makubwa yatatokea Mashariki ya Kati hivi sasa. Na muhimu sana, bei ya mafuta inabwaga chini, , na soko la hisa linapanda kama roketi leo," Trump alinukuliwa na PBS News akisema Jumatatu mjini Evian, Ufaransa, ambako Mkutano wa Viongozi wa G7 unafanyika.
Kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kusimamishwa kwa operesheni za kijeshi katika maeneo mbalimbali ya mstari wa mbele kunatangazwa na pande zote mbili, lakini pande mbili zinaendelea kubishana katika maelezo yao kuhusu mambo muhimu. Moja kati ya masuala ambayo hayajatatuliwa ni ada zilizopendekezwa na Iran kwa meli zinazopitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Trump alisisitiza Jumatatu kwamba mlango-bahari huo utakuwa usio na tozo za ada na "hakuna mabishano juu ya hilo."
Hata hivyo, shirika la habari la Fars la Iran liliripoti Jumatatu kwamba Iran itakubali kupita kwa meli kupitia njia hiyo ya maji bila malipo ndani ya siku 60 tu, baada ya hapo nchi hiyo inapanga kutoa huduma za usalama, mambo ya baharini, mazingira na bima kwa meli zinazovuka mpaka, na itatumia mapato husika kwa maendeleo ya uchumi wake.
Tofauti pia zinabaki juu ya suala la Lebanon. Pande zote mbili zilitangaza kusimamisha mapigano mara moja katika mistari yote ya mbele, lakini bado hazijaeleza wazi mpango huo utahitaji jeshi la Israeli kuondoka kutoka maeneo makubwa ya kusini mwa Lebanon ambayo linayashikilia kwa sasa.
Juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, pande zote mbili zimesema, Iran imeahidi kutofanya utafiti na kutotengeneza silaha za nyuklia, lakini zimetoa madai tofauti kuhusu uondoaji wa uraniamu iliyorutubishwa sana ya Iran.
Pande zote mbili pia zinatoa madai yanayokinzana kuhusu makubaliano juu ya masuala ya mali zilizozuiliwa na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran.
Wataalamu wanasema kwamba kutokana na maelezo yaliyotolewa hadi sasa, makubaliano hayo hayajatatua kimsingi migongano ya muda mrefu kati ya Marekani na Iran juu ya masuala kuhusu mpango wa nyuklia, wala hayajapunguza hali ya kutoaminiana kati ya pande hizo mbili.

Picha hii iliyopigwa Aprili 11, 2026 ikionyesha hali ya nje ya kituo cha waandishi wa habari kwa ajili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran mjini Islamabad, Pakistan. (Xinhua/Wang Shen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



