Lugha Nyingine
Mwaka mmoja baadaye, urithi wa daktari Mchina Zhang Junqiao unaendelea kuishi nchini Tanzania

Madaktari wa ganzi wenyeji wakikagua sanduku la vifaa tiba lenye maandishi ya mkono ya jina na namba ya simu ya marehemu daktari Mchina Zhang Junqiao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, Tanzania, Mei 29, 2026. (Xinhua/Ding Ting)
DAR ES SALAAM – Ndani ya chumba cha upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, Tanzania, sanduku la vifaa tiba la aluminiamu limewekwa tuli kwenye kona.
Kilichoandikwa kwenye kifuniko chake kwa alama nyeusi ni maneno matatu rahisi: " Dr. ZHANG (Dk. ZHANG)," " CHINA TEAM (TIMU YA CHINA)," na namba ya simu.
Maandishi hayo ya mkono yamefifia baada ya muda. Namba hizo za simu hazifanyi kazi tena. Lakini hakuna mtu aliyeifuta.
"Tunataka maneno haya yabaki hapa milele," amesema Hosea Boniface, daktari wa ganzi katika hospitali hiyo, akigusa sanduku hilo kilaini.
Sanduku hilo hapo awali lilikuwa la Zhang Junqiao, daktari Mchina ambaye alihudumu nchini Tanzania akiwa kiongozi wa kundi la 27 la timu ya madaktari ya China. Juni 15, 2025, Zhang alifariki wakati akimwokoa mwanamke Mtanzania kutoka baharini jijini Dar es Salaam. Alikuwa na umri wa miaka 38.
Mwaka mmoja baadaye, nyayo za uwepo wake zinabaki kote Tanzania, katika korido za hospitali, katika kumbukumbu za wenzake, katika maisha ya watoto aliowasaidia, na katika mioyo ya watu ambao kamwe hawasahau wema wake.
Katika hospitali, ambako Zhang alitumia muda wake mwingi kuwafunza madaktari vijana wa ganzi, wafanyakazi wenzake bado wanamzungumzia kwa pongezi.
“Kamwe hakuchoka kujibu maswali yetu," amekumbushia Boniface. "Wakati mwingine alikuwa akionyesha utaratibu uleule kwa kurudia tena na tena hadi tutakapoelewa kikamilifu."
Tanzania inakabiliwa na uhaba sugu wa madaktari wa ganzi waliofunzwa, na Zhang alitumia muda wake mwingi kuwajengea uwezo wahudumu wenyeji wa afya, amesema Boniface, akiongeza kuwa madaktari wengi vijana aliowafunza sasa wanaweza kufanya operesheni ambazo hapo awali zilihitaji wataalamu wa kigeni.
Mbali kutoka hospitalini, Zhang anakumbukwa kwa njia zingine.
Kila jioni, watoto wanaouza maputo hupita kwenye msongamano wa magari kando ya barabara za Dar es Salaam zenye pilika nyingi za ufukweni mwa bahari. Miongoni mwao ni Nefat mwenye umri wa miaka tisa, ambaye bado anamkumbuka daktari huyo Mchina ambaye mara nyingi alisimamisha baiskeli yake kuzungumza naye.
"Alikuwa akiuliza kama tumekula na ni maputo mangapi tumeuza," amesema.
Katika kumbukumbu yake, daktari huyo Mchina alikuwa na tabasamu usoni mwake kila wakati. "Magari mengi yalitupita, lakini hakuna aliyesimama," Nefat amesema, akiinamisha kichwa chake, "Lakini yeye alisimama."
Aliposikia kuhusu kifo cha Zhang, alilia kwa siku nyingi.
"Nilidhani ningeweza kumwona tena siku moja," amesema kwa upole.
Mike, mpiga picha wa ufukweni, aliona umati wa watu ukikusanyika kando ya ufukwe na akakimbilia kwenye mkusanyiko, akielezea kwamba katika mawimbi makali, jamaa Mchina alikuwa akijitahidi kumrudisha mahali salama mwanamke aliyekuwa akizama.
"Bahari ilikuwa na mawimbi, na alikuwa amechoka, lakini aliendelea," Mike amekumbushia.
Aliinua kamera yake na kubonyeza kitufe cha kupiga picha.
Picha hiyo ilimwonyesha Zhang akiwa amemshikilia mwanamke huyo juu ya maji, akipambana na mawimbi wakati alipokuwa akielekea ufukweni. Mwanamke huyo alinusurika, Zhang hakunusurika.
Wakati huo, Mike hakujua jina la jamaa huyo wala taaluma yake.
"Lakini nilijua jambo moja," amesema. "Alikuwa akiokoa maisha."
"Alikuwa zawadi kutoka kwa Mungu kwa watu wa Tanzania," Mike amesema. "Sio kila mtu angefanya hivyo, lakini alifanya hivyo."
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Zhang aliandika kwenye mtandao wa kijamii: "Kuhudumia watu hakujui mipaka. Kama daktari Mchina, ninajivunia nchi yangu na taaluma yangu."

Liu Jia (Kulia), kiongozi wa kundi la 28 la timu ya madaktari ya China nchini Tanzania, akizungumza na daktari wa ganzi mwenyeji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, Tanzania, Juni 11, 2026. (Picha na Lin Guangyao/Xinhua)

Daktari Mchina marehemu Zhang Junqiao akipiga picha na watoto wenyeji, Zanzibar, Tanzania, Desemba 26, 2024. (Xinhua)

Picha iliyopigwa Oktoba 12, 2024 ikimwoonyesha daktari Mchina marehemu Zhang Junqiao akichangia damu kwenye kampeni ya kuchangia damu kwa hiari nchini Tanzania. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



