Lugha Nyingine
Wagonjwa wa Ebola nchini DRC waongezeka hadi 837 huku juhudi za kukabiliana zikikabiliwa na hali isiyo ya usalama na upingaji wa jamii

Mfanyakazi wa afya akiwa amemkumbatia mgonjwa aliyepona kwenye kituo cha matibabu ya Ebola, huko Rwampara, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 16, 2026. (Xinhua)
KINSHASA - Idadi ya wagonjwa wa Ebola waliothibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeongezeka hadi 837, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu 196, huku mamlaka za afya na washirika wa kimataifa wakionya kwamba mlipuko huo unazidi kuwa mbaya kutokana na maambukizi ya mara kwa mara ndani ya jamii na kupanuka kijiografia.
Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na wizara ya afya ya DRC, vifo vya wagonjwa vimefikia asilimia 23.4, huku jumla ya wagonjwa 49 wakiwa wamepona, wakati huohuo wagonjwa 376 bado wako katika hali ya kujitenga.
Mlipuko huo uliosababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, bado unatokea zaidi katika maeneo makubwa yenye maambukizi mengi, hasa Bunia, Mongbwalu na Rwampara katika jimbo la Ituri.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa juzi Jumanne na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtawanyiko wa kijiografia wa kanda za afya zilizoathiriwa unapanuka, maambukizi yanaendelea katika maeneo ya mazingira ya mijini na migodini, ufuatiliaji wa watu waliokutana na watu wanaoshukiwa kuambukizwa katika baadhi ya majimbo haujafikia hali ya kutarajiwa, na hali isiyo ya usalama inaendelea katika maeneo yaliyoathiriwa, vyote hivyo vinaendelea kuathiri shughuli za kukabiliana na ugonjwa huo na kuongeza hatari ya kuenea zaidi ndani ya DRC na nchi jirani.
WHO imesema kwamba mlipuko huo unazidi kuwa mbaya, maambukizi yanaendelea kuenea ndani ya maeneo ya wakazi, idadi ya wagonjwa na vifo vya watu inaongezeka, na kupanuka kijiografia kunaendelea katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini. Ripoti hiyo ya WHO imesema kusambaa kwa ugonjwa huo katika maeneo mapya yaliyoathiriwa kunaonyesha kupanuka kunakoendelea zaidi katika maeneo ya awali yenye maambukizi zaidi.
Katika nchi jirani ya Uganda, kwa mujibu wa WHO, hakuna wagonjwa wapya wanaothibitishwa katika wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo. Hata hivyo, WHO imesema uhusiano unaoendelea wa kiepidemiolojia na maambukizi nchini DRC unasisitiza hatari inayoendelea ya kusambaa kwa ugonjwa kuvuka mipaka na maambukizi ya pili.
Uganda imeripoti wagonjwa 19 waliothibitishwa, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu wawili, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vilisema Jumanne katika taarifa mpya ya kila siku.
Katika Jimbo la Kivu Kaskazini, mamlaka za afya za jimbo hilo zimesema kwamba mwanamke aliyepimwa na kukutwa na Ebola na mtoto wake walichukuliwa Jumatatu usiku na "wanaume wenye silaha". WHO imesema kwamba juhudi za kukabiliana na Ebola bado zinaendelea kuzuiliwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na upingaji wa jamii katika maeneo yaliyoathiriwa.
DRC ilitangaza duru mpya ya mlipuko huo wa Ebola Mei 15. Maeneo yaliyoathiriwa yako mashariki mwa nchi hiyo iliyokumbwa na migogoro, ambapo vurugu za kutumia silaha, watu kukimbia makazi yao na miundombinu dhaifu ya afya vimeleta changamoto sugu katika kukabiliana na janga hilo.

Mfanyakazi wa afya akinawa mikono yake kwenye kituo cha matibabu ya Ebola, huko Rwampara, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 16, 2026. (Xinhua)

Wafanyakazi wa afya wakikausha glavu zilizosafishwa kwa dawa za kuua vijidudu kwenye kituo cha matibabu ya Ebola, huko Rwampara, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 16, 2026. (Xinhua)

Mfanyakazi wa afya akinyunyuzia gari dawa kuua vijidudu kwenye kituo cha matibabu ya Ebola, Rwampara, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 16, 2026. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



