Maonyesho ya mashine za ujenzi yafunguliwa nchini Kenya

(CRI Online) Juni 18, 2026

Maonyesho ya Kimataifa ya Mashine za Ujenzi Afrika ya mwaka 2026 yameanza jana Jumatano katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kukutanisha maofisa wa serikali, wamiliki wa biashara na watengenezaji kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiviwanda kati ya China na Afrika.

Maonyesho hayo ya siku tatu yalioandaliwa kwa pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji ya Kenya na Maonyesho ya Kimataifa ya Mashine za Ujenzi ya Hunan Hongxing, yamevutia zaidi ya viwanda 200 kutoka China na Afrika, ikiwemo wajumbe wa wafanyabiashara kutoka Manispaa ya Chongqing iliyoko kusini magharibi mwa China.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo, katibu mkuu katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda nchini Kenya, Juma Mukhwama amesema, maonyesho hayo ni kielelezo cha kuaminika kwa Kenya kama kituo cha uwekezaji na yanaonyesha kupanuka kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Afrika na jamii ya utengenezaji duniani.

Kwa upande wake, meneja mkuu wa Maonyesho ya Kimataifa ya Mashine za Ujenzi ya Hunan Hongxing, Ding Guiping amesema, maonyesho hayo yanatumika kama jukwaa la kutekeleza matokeo ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha