Lugha Nyingine
Mamlaka za Afrika Kusini zatuma maelfu ya polisi kukabiliana na maandamano ya kitaifa ya kupinga uhamiaji

Picha iliyopigwa Juni 30, 2026 ikionyesha waandamanaji wakiandamana kwenye maandamano makubwa dhidi ya uhamiaji haramu jijini Johannesburg, Afrika Kusini (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
JOHANNESBURG - Mamlaka za Afrika Kusini zilituma maelfu ya maafisa wa polisi jana Jumanne wakati maandamano dhidi ya uhamiaji haramu yalikuwa yakifanyika kote nchini humo chini ya hatua kali za ulinzi.
Maandamano yaliripotiwa katika miji kadhaa mikubwa, ikiwemo Johannesburg, Pretoria, Cape Town na Durban. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, waandamanaji zaidi ya 10,000 walikuwa wakitarajiwa kukusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa mjini Pretoria, mji mkuu wa utawala wa nchi hiyo. Hapo awali, Idara ya Polisi ya Jiji la Johannesburg ilisema maandamano matatu ya kupinga jijini Johannesburg yameidhinishwa, huku mahudhurio pia yalikuwa yakitarajiwa kuzidi 10,000.
Wizara ya Polisi ya Afrika Kusini imesema kwamba ingawa maandamano mengi yalikuwa ya amani, polisi walikabiliana na matukio machache ya uhalifu. Imeonya kwamba mtu yeyote anayejaribu kutumia vibaya maandamano hayo kufanya uhalifu atakabiliwa na hatua kali za kusimamia utekelezaji wa sheria.
Kabla ya maandamano hayo, Kamishna wa Polisi wa Jimbo la Gauteng, Tommy Mthombeni, alisema maafisa takriban 13,000 wa Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini, maafisa zaidi ya 10,000 wa polisi wa miji, walinzi wa trafiki wapatao 8,000 na wafanyakazi zaidi ya 217,000 wa usalama binafsi walihamasishwa kufuatilia maandamano hayo na kudumisha utulivu wa umma.
Maandamano hayo yalifuatia wiki kadhaa za uhamasishaji kutoka kwa makundi yanayopinga uhamiaji, likiwemo kundi la "March and March" vilevile Operesheni Dudula, miongoni mwa mengine.
Waandaaji wanasema wanapinga kile wanachokieleza kuwa ni kushindwa kwa serikali kushughulikia uhamiaji haramu, kudai udhibiti mkali zaidi wa mipaka, kufukuzwa haraka zaidi kwa wahamiaji wasio na vibali, hatua kali za kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji, na kuwapa kipaumbele raia wa Afrika Kusini katika fursa za ajira na huduma za umma.
Maandamano hayo yalivuruga shughuli za kawaida katika sehemu za Johannesburg, ikiwa ni pamoja na Hillbrow, Alexandra, Tembisa na Soweto. Baadhi ya biashara zilifungwa kwa muda kama sehemu ya tahadhari, wakati huohuo waendesha shughuli za usafiri wa umma wameripoti idadi ndogo ya abiria.
Mivutano inayozidi kuongezeka kuhusiana na maandamano hayo ya kitaifa nchini Afrika Kusini pia imesababisha serikali kadhaa za Afrika kutoa ushauri wa usalama. Katika wiki za hivi karibuni, Malawi, Zimbabwe, Msumbiji, Nigeria, Ghana na Uganda zimetoa wito kwa raia wao walioko Afrika Kusini kuendelea kuwa macho, huku baadhi ya serikali zikitoa usaidizi wa kuwarudisha nyumbani kwa hiari wale wanaotaka kurudi nyumbani.
Serikali ya Afrika Kusini imekuwa mara kwa mara ikikataa hatua hizo za kuwa macho, ikisisitiza kwamba kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji ni jukumu la mamlaka za serikali.
Katika jarida lake la wiki lililochapishwa Jumatatu wiki hii, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitoa wito kwa Waafrika Kusini kutumia haki yao ya kikatiba ya kuandamana kwa amani wakati huohuo alionya kwamba vurugu, vitisho na kujichukulia sheria mkononi havitavumiliwa wakati wa maandamano.

Waandamanaji wakiandamana kwenye maandamano makubwa dhidi ya uhamiaji haramu jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Juni 30, 2026. (Picha na Shiraaz Mohamed/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



