Lugha Nyingine
Waziri wa utalii wa Ushelisheli asema uhusiano kati ya Ushelisheli na China utaimarika zaidi katika kipindi cha miaka 50 ijayo

Waziri wa Utalii na Utamaduni wa Ushelisheli Amanda Bernstein akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua mjini Victoria,Ushelisheli, Juni 25, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)
VICTORIA - Waziri wa Utalii na Utamaduni wa Ushelisheli Amanda Bernstein amesema uhusiano kati ya Ushelisheli na China sasa unaingia katika zama mpya ya ushirikiano na maendeleo, hasa katika mawasiliano ya kitamaduni.
"Uhusiano wetu umekuwa ukiimarika zaidi na zaidi. China daima imekuwa mshirika mkubwa kwa Ushelisheli," Bernstein hivi karibuni ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua mjini Victoria, mji mkuu wa Ushelisheli.
Ikiwa ni nchi ya kwanza ya Afrika kusaini makubaliano juu ya kusameheana mahitaji ya visa na China, Ushelisheli, yenye uzuri wake wa kipekee wa mazingira asilia na utamaduni wa Creole, imeshuhudia shauku inayozidi kuongezeka kutoka kwa watalii wa China katika miaka ya hivi karibuni, ikitoa uzoefu wa kipekee wa utalii wakati huohuo ikiacha nafasi kubwa ya kupanua mabadilishano ya pande mbili, waziri huyo amesema.
Huku mwaka 2026 ni wa maadhimisho ya Mwaka wa Mwasilianokati ya Watu wa China na Afrika, Bernstein amezungumzia hasa utalii kuwa ni " diplomasia ya dhati kabisa," ambayo inawezesha watu kutoka nchi tofauti "kujionea tamaduni za kila mmoja kihalisia," na hivyo kujenga kuelewana na kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili.
Waziri huyo amesema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuwaleta watu wa Ushelisheli na China karibu zaidi na kuhimiza kufunzana, akiongeza kuwa kuimarisha uhusiano kati ya Ushelisheli na China si tu kunufaisha maendeleo ya utalii, bali pia kutawezesha mabadilishano na ushirikiano wa pande mbili.

Picha hii ikionyesha mandhari ya ufukwe (chini) kwenye Kisiwa cha Mahe, Ushelisheli, Juni 29, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)
“Kadiri watu wa nchi hizi mbili wanavyozidi kuwa karibu zaidi, ndivyo watakavyonufaika zaidi na ndivyo uthamini na uelewa wa tamaduni za kila mmoja wao utakavyokuwa imara zaidi,” Bernstein amesema.
Kwa kuwa Ushelisheli ni nchi ndogo ya kisiwa inayoendelea inayokabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabianchi na shinikizo za mazingira, waziri huyo amesema nchi hiyo inabaki kuwa na dhamira ya kuendeleza tasnia yake ya utalii "kwa njia endelevu sana" wakati huohuo ikilinda rasilimali zake na kuepuka matumizi kupita kiasi.
"Uendelevu uko kwenye kiini cha maamuzi yetu yote ya kisera kuhusu utalii," Bernstein amesema, akiongeza kuwa nchi hiyo inatarajia kuimarisha ushirikiano na washirika, ikiwemo China, katika kuunga mkono malengo yake ya maendeleo.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Ushelisheli na China zimepata matokeo halisi kupitia ushirikiano katika mipango mbalimbali, ikiwemo uhifadhi wa utamaduni vilevile miradi ya mazingira na miundombinu. Amesema, uwezekano wa ushirikiano wa pande mbili unaenea zaidi ya utalii wa kawaida wa mapumziko hadi maeneo kama vile utalii wa ikolojia.
Wakati huu ambapo nchi hizo mbili zikisherehekea Jumanne hii maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia, Bernstein ameeleza matumaini yake kuhusu miaka 50 ijayo ya uhusiano wa pande mbili.
"Nina imani kubwa kwamba tutaendelea kuuona uhusiano huu dhati ukiimarika zaidi katika kipindi cha miaka 50 ijayo," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



