Lugha Nyingine
Kutumikia Watu Kupitia Kikombe cha Kahawa
Ndani ya duka la kahawa katika Wilaya ya Menglian, mkoani Yunnan, China, Zhao Hua yuko anatengeneza kwa umakini kahawa ya kuchuja kwa mkono.
Wazazi wa Zhao Hua walikuwa miongoni mwa wakulima wa mapema kabisa kuanza kupanda kahawa wilayani humo. "Baba yangu alilima kahawa maisha yake yote, lakini yeye mwenyewe hakuwahi hata kuonja kikombe kimoja cha kahawa yake. Hakujua mahali maharagwe hayo machungu ya kahawa yalikuwa yakiishia, alichojua tu ni kwamba mtu fulani alikuwa akija kuyanunua, na aliweza kupata fedha kutokana nayo," alisema Zhao Hua.
Hivi sasa, duka lake hilo la kahawa ni moja ya maduka yanayopendwa zaidi kwenye "Mtaa wa Kahawa Bora" ya Menglian. Video zake fupi anazozirekodi na kuzichapisha mitandaoni zimewafanya watu wengi zaidi kuufahamu mji huo mdogo wa mpakani pamoja na kahawa yake. Aidha, maharagwe yake ya kahawa sasa yanauzwa kwenye masoko ya nje kama vile Japani na Australia kupitia mawakala.
Nyuma ya mabadiliko haya, ni mabadiliko katika hatma ya mji huu.
Uhusiano kati ya Menglian na kahawa ulianza tangu mwaka 1958, huku upandaji wa zao hilo kwa kiwango kikubwa ukianza katika miaka ya 1980. Li Meiying, Katibu wa Chama na Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo ya Sekta ya Chai na Viumbe cha Menglian, bado anakumbuka alivyokuwa akiona makada na wakulima wakifanya kazi pamoja mashambani wakati akiwa njiani kuelekea shuleni akiwa mtoto, leo hii, mashamba makubwa ya kahawa yanafunika milima na tambarare ya eneo hilo.
Mwaka 2023, wakati "Mtaa wa Kahawa Bora" ya Menglian ulipofunguliwa kwa mara ya kwanza, wakulima na wamiliki wa maduka walikuwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake. Li Meiying na wenzake walikuwa wakienda kusaidia kuangalia maduka ya jirani na kuhudumia wateja baada ya kazi.
Baadaye, wakati serikali ya wilaya hiyo ilipoandaa kushiriki kwenye maonesho ya kibiashara katika mji mwingine, Li haraka sana alimfikiria Zhao Hua. "Vijana hawa ni wazuri sana katika kueleza simulizi za kahawa yetu ya kienyeji. Kwa kahawa ya Menglian kwenda nje kuwafikia wateja duniani, inahitaji mawazo mazuri na ubunifu mpya wa vijana," alisema Li. Ili kuvutia vijana wengi zaidi kurudi nyumbani kwa asili yao, wilaya hiyo ya Menglian imeanzisha mradi wa "Jumuiya ya Wasafiri wa Kidijitali".
"Kufanya kila jambo dogo kwa umakini na kwa ubora, ndiyo tafsiri nzuri zaidi ya ‘Kutumikia Watu’," alisema Li Meiying.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



